Kuutazama Ulimwengu
“Mnamo Januari (Mwezi wa 1) 2009, nchi nane zilikuwa na zaidi ya silaha 23 300 za nyuklia kwa ujumla.”—TAASISI YA KIMATAIFA YA UTAFITI WA AMANI YA STOCKHOLM, SWEDEN.
Maelfu ya visima na pampu za maji za Afrika, ambazo nyingi zilijengwa hivi karibuni kwa msaada kutoka nchi za kigeni, zimeharibika “kwa sababu ndogo na inayoweza kuepukika: hazitunzwi.”—TAASISI YA KIMATAIFA YA MAZINGIRA NA MAENDELEO, UINGEREZA.
Wanasayansi Wachunguza Mtoto wa Mamothi
Wanasayansi Warusi wamepiga picha zinazoonyesha mambo mengi kuhusu viungo vya ndani ya mamothi (mnyama mkubwa sana anayefanana na tembo). Mnyama huyo, ambaye alikuwa na umri wa miezi mitatu au minne alipokufa, alipatikana chini ya barafu kwenye eneo la Yamalo-Nenets lililo kwenye Aktiki ya Urusi. Alexei Tikhonov, naibu-msimamizi wa Taasisi ya Sayansi ya Zuolojia ya Urusi alisema kwamba “hayo ndiyo mabaki ya mnyama wa kale zaidi yaliyohifadhiwa vizuri zaidi.” Eksirei za kompyuta kama zile zinazotumiwa kuwachunguza wanadamu, zilionyesha kwamba mnyama huyo hakuwa na majeraha yoyote. Kwa kuwa mfumo wake wa kupitishia hewa na wa kumeng’enya chakula ulikuwa “umezibwa” kwa kile kinachoonekana kuwa mchanga-tope, wanasayansi walifikia mkataa kwamba mnyama huyo “alikufa baada ya kuzama.”
Talaka ya Moja kwa Moja
Hivi karibuni imekuwa rahisi zaidi kupata talaka huko Mexico City, linaripoti gazeti El Universal. Mnamo 2008, zile sababu 21 zilizohitajika ili mtu apate talaka, yaani, kukosa uaminifu, jeuri, na kadhalika, ziliondolewa katika vitabu vya sheria. Sasa mtu anahitaji tu kulipa dola 400 hivi (za Marekani) kwenye benki ya ofisi ya sheria na kutuma mahakamani fomu ya ombi iliyotiwa sahihi ambayo inaweza kupatikana kwenye Intaneti, akisema tu kwamba hampendi mwenzi wake. Mtu hahitaji kuthibitisha lolote mbele ya hakimu. Unaweza kupata talaka baada ya miezi miwili hadi minne tu. Hiyo ni tofauti na ilivyokuwa chini ya mfumo wa awali kwani mtu alihitaji kusubiri kwa miaka kadhaa. Ruhusa ya kuwalea watoto, malipo ya talaka, kugawana mali, na mambo mengi hutatuliwa baadaye.
Ndege Wavumaji—‘Wanasonga Kasi Kuliko Ndege za Vita’
Mtafiti katika Chuo Kikuu cha California, huko Berkeley, Marekani anasema kwamba mwendo ambao ndege mvumaji husonga kwa sekunde unapokadiriwa kwa urefu wa mwili wake na kulinganishwa na ndege ya vita, inaonekana kwamba ndege mvumaji husonga kwa kasi zaidi. Christopher Clark alichukua video ya ndege hao wakichumbiana na kukadiria kwamba waliporuka kuelekea chini ili kuwavutia ndege wa kike, “kwa kila sekunde ndege hao [wa kiume] waliruka umbali unaozidi urefu wa mwili wao kwa mara 400 hivi.” Clark anasema kwamba mwendo huo “ni wa kasi zaidi kuliko ndege ya vita” inaposonga kwa mwendo wake wa kasi zaidi. Anapoanza kujaribu kujirudisha juu, ndege huyo hukabiliwa na nguvu zinazozidi nguvu za uvutano kwa zaidi ya mara kumi, na huo ni uvutano mwingi zaidi kuliko ule ambao marubani wa ndege za vita wanaweza kustahimili bila kupoteza fahamu.