Kuutazama Ulimwengu
“Zaidi ya nusu ya watu nchini Urusi wanafikiri kwamba kuwahonga maofisa ndiyo njia bora zaidi ya ‘kutatua matatizo.’”—SHIRIKA LA HABARI LA REUTERS, URUSI.
“Kulingana na makadirio mapya ya Shirika la Usalama wa Kitaifa, angalau asilimia 28 ya aksidenti za barabarani nchini Marekani, yaani, aksidenti milioni 1.6 kila mwaka, zinasababishwa na madereva wanaozungumza kwenye simu za mkononi, au wanaotuma na kusoma ujumbe.”—UC BERKELEY WELLNESS LETTER, MAREKANI.
“Uchunguzi mmoja ulionyesha kwamba asilimia 17.5 ya watu wazima nchini China wana matatizo ya akili . . . Ni rahisi zaidi kwa wanawake kuwa na tatizo la kubadilika-badilika kwa hisia na tatizo la kuwa na wasiwasi mwingi, kuliko wanaume.”—CHINA DAILY, CHINA.
“Historia Isiyopendeza”
Gazeti The Irish Times linasema kwamba“Ripoti ya Tume ya Uchunguzi Kuhusu Kuwatendea Watoto Vibaya inafunua historia isiyopendeza ya Ireland.” Kulingana na gazeti hilo, ripoti hiyo inafichua historia ya watoto kutendewa vibaya katika taasisi za kidini za Wakatoliki, ambako kulitia ndani “kuwachapa watoto waliopatikana na hatia ya kuwa na chawa vichwani,” na pia kuwatendea vibaya kingono. Matendo hayo yalipuuzwa kwa sababu ya ushikamanifu usiofaa kwa “mamlaka kuu ya Kanisa Katoliki,” linasema gazeti hilo. “Aibu Kubwa kwa Serikali na Kanisa,” ndicho kilichokuwa kichwa kikuu katika gazeti hilo, likinukuu maneno ya mtu mmoja aliyewasikitikia waliotendewa vibaya.
Maji Kwenye Mwezi
Wanasayansi waliorusha roketi kwenye mwezi wanasema kwamba vumbi lililotokezwa wakati roketi hiyo ilipotua lilikuwa na maji. Wingu hilo la vumbi lilichunguzwa kwa vifaa vinavyochanganua muundo wa chembe kwa kutenganisha kiwango cha nuru kinachofyonzwa au kutokezwa na chembe hizo. “Tunafichua mambo yasiyojulikana ya jirani wetu wa karibu katika mfumo wa jua,” akasema Michael Wargo, mwanasayansi mkuu wa kuchunguza mwezi katika makao makuu ya NASA huko Washington, D.C. Hivi karibuni zaidi, uchunguzi umeonyesha kwamba kuna mamilioni ya tani za maji kwenye ncha ya kaskazini ya mwezi.
Mashini Inayouza Dhahabu
Katika maeneo kadhaa ulimwenguni, dhahabu inaweza kupatikana katika mashini ya kuuzia vitu. Kwa mfano, hoteli fulani huko Abu Dhabi, katika Muungano wa Falme za Kiarabu, ina mashini inayouza bidhaa 320, kutia ndani dhahabu yenye uzito wa gramu 10 na pia sarafu za pekee za dhahabu. Bei ya dhahabu hiyo hubadilishwa baada ya kila dakika kumi, kwa kutumia mtandao wa kompyuta uliounganishwa kwenye soko la kimataifa. Mwanzoni, mashini hiyo ilikubali pesa za nchi hiyo tu, lakini sasa watengenezaji wake wanapanga kufanya ikubali kadi za mkopo. Ripoti ya Shirika la Habari la Reuters inasema kwamba mashini hiyo iliwekwa katika nchi hiyo “kwa sababu watu wengi katika eneo hilo wanapenda kununua dhahabu.”