Je, Utajiri wa Mfalme Sulemani Umetiwa Chumvi?
“Uzani wa dhahabu iliyomfikia Sulemani mwaka mmoja, ndio talanta mia sita sitini na sita.”—1 Wafalme 10:14.
KULINGANA na mstari huo wa Biblia, Mfalme Sulemani alipata tani zaidi ya 25 za dhahabu katika mwaka mmoja! Leo hiyo ingekuwa yenye thamani ya dola 240,000,000. Hiyo ni karibu mara mbili ya kiasi cha dhahabu kilichochimbwa ulimwenguni pote katika mwaka wa 1800. Je, hilo lawezekana? Uthibitisho wa kiakiolojia waonyesha nini? Huo wadokeza kwamba rekodi ya Biblia juu ya utajiri wa Sulemani kwa hakika ni jambo liwezalo kuaminika. Jarida Biblical Archaeology Review lasema hivi:
◻ Mfalme Thutmose wa 3 wa Misri (mileani ya pili K.W.K.) alitolea hekalu la Amon-Ra katika Karnak, karibu tani 13.5 za vitu vya dhahabu—na hivyo vilikuwa sehemu tu ya hiyo zawadi.
◻ Miandiko ya Kimisri yarekodi zawadi za jumla ya karibu tani 383 za dhahabu na fedha ambazo Mfalme Osorkon wa 1 (mapema katika mileani ya kwanza K.W.K.) alitolea miungu.
Zaidi ya hayo, lile buku Classical Greece la mfululizo Great Ages of Man laripoti hivi:
◻ Machimbo ya Pangaeum katika Thrasi yalimtolea Mfalme Philip wa 2, (359-336 K.W.K.) tani zaidi ya 37 za dhahabu kila mwaka.
◻ Wakati Aleksanda Mkuu (336-323 K.W.K.), mwana wa Philip, alipoliteka Susa, jiji kuu la milki ya Uajemi, hazina zipatazo tani zaidi ya 1,000 za dhahabu zilipatikana.—The New Encyclopædia Britannica.
Kwa hiyo ufafanuzi wa Biblia juu ya utajiri wa Mfalme Sulemani si jambo lisilo halisi. Kumbuka pia kwamba Sulemani ‘aliwapita wafalme wote wa duniani kwa mali’ wakati huo.—1 Wafalme 10:23.
Sulemani alitumiaje utajiri wake? Kiti chake cha ufalme kilifunikwa kwa “dhahabu iliyo safi,” na vyombo vyake vya kunywea vilikuwa “vya dhahabu,” na alikuwa na ngao kubwa 200 na vigao 300 vya “dhahabu iliyofuliwa.” (1 Wafalme 10:16-21) Zaidi ya yote, dhahabu ya Sulemani ilitumiwa kuhusiana na hekalu la Yehova katika Yerusalemu. Vinara vya taa vya hekalu na vyombo vitakatifu, kama vile nyuma, mabakuli, mitungi, na makarai, vilifanyizwa kwa dhahabu na fedha. Wale makerubi wenye urefu wa meta 4.5 waliokuwa katika Patakatifu Zaidi, ile madhabahu ya uvumba, na hata sehemu yote ya ndani ya ile nyumba ilifunikwa kwa dhahabu.—1 Wafalme 6:20-22; 7:48-50; 1 Mambo ya Nyakati 28:17.
Namna gani hekalu lenye kufunikwa kwa dhahabu? Kwa kupendeza, utumizi wa dhahabu wa jinsi hiyo haukuwa kwa vyovyote jambo lisilo la kawaida katika ulimwengu wa kale. Jarida Biblical Archaeology Review laonyesha kwamba Amenophis wa 3 wa Misri “alimheshimu yule mungu mkubwa Amun kwa kumtolea hekalu katika Thebes ‘lililofunikwa kwa dhahabu kotekote, sakafu yalo ikiwa imepambwa kwa fedha, [na] viingilio vyalo vyote kwa elektramu’”—mchanganyiko wa dhahabu na fedha. Zaidi ya hayo, Esar-haddon wa Ashuru (karne ya saba K.W.K.) alifunika milango na kutanda kuta za mahali patakatifu pa Ashur kwa dhahabu. Kuhusu hekalu la Sin katika Harani, Nabonido wa Babiloni (karne ya sita K.W.K.) alirekodi hivi: “Nilifunika kuta zalo kwa dhahabu na fedha, na kuzifanya zing’ae kama jua.”
Hivyo, rekodi za kihistoria zadokeza kwamba simulizi la Kibiblia la utajiri wa Mfalme Sulemani halikutiwa chumvi.