Sura Ya Kumi Na Nne
Wale Wafalme Wawili Wabadilika
1, 2. (a) Ni nini kilichomfanya Antiochus wa Nne akubali madai ya Roma? (b) Siria ilipata kuwa mkoa wa Roma lini?
MTAWALA wa Siria Antiochus wa Nne avamia Misri na kujitawaza mwenyewe kuwa mfalme. Mfalme Ptolemy wa Sita wa Misri aombapo msaada, Roma yamtuma Balozi Caius Popilius Laenas aende Misri. Aenda na meli nyingi zenye kuvutia na maagizo kutoka kwa Seneti ya Roma kwamba Antiochus wa Nne akane ufalme wake wa Misri na kutoka nchini humo. Mfalme wa Siria na balozi wa Roma wakutana ana kwa ana Eleusis, kitongoji cha Aleksandria. Antiochus wa Nne aomba wakati ili apate kushauriana na washauri wake, lakini Laenas achora duara kumzunguka mfalme na kumwambia ajibu kabla ya kuvuka mstari huo. Akiwa ameaibishwa, Antiochus wa Nne akubali madai ya Roma na kurudi Siria mwaka wa 168 K.W.K. Ndivyo uishavyo ushindani kati ya mfalme wa kaskazini wa Siria na mfalme wa kusini wa Misri.
2 Ikiwa na fungu kubwa katika mambo ya Mashariki ya Kati, Roma yaendelea kutawala Siria. Kwa sababu hiyo, ingawa wafalme wengine wa nasaba ya Seleuko walitawala Siria baada ya Antiochus wa Nne kufa mwaka wa 163 K.W.K., hawapati kuwa “mfalme wa kaskazini.” (Danieli 11:15) Hatimaye Siria inakuwa mkoa wa Roma mwaka wa 64 K.W.K.
3. Roma ilipata mamlaka kuliko Misri lini na jinsi gani?
3 Nasaba ya Ptolemy ya Misri yaendelea kuwa “mfalme wa kusini” kwa zaidi ya miaka 130 baada ya Antiochus wa Nne kufa. (Danieli 11:14) Wakati wa vita ya Actium, mwaka wa 31 K.W.K., mtawala wa Roma Octavian ayashinda majeshi ya muungano ya malkia wa mwisho wa nasaba ya Ptolemy—Kleopatra wa Saba—pamoja na mpenzi wake Mroma, Mark Antony. Baada ya Kleopatra kujiua mwaka uliofuata, Misri pia yawa mkoa wa Roma na kukoma kuwa mfalme wa kusini. Mwaka wa 30 K.W.K., Roma ina mamlaka kuu kuliko Siria na Misri. Je, sasa tutarajie tawala nyingine ziwe mfalme wa kaskazini na mfalme wa kusini?
MFALME MPYA ATUMA ‘MTOZA-USHURU’
4. Kwa nini tutarajie utawala mwingine uwe mfalme wa kaskazini?
4 Masika ya mwaka wa 33 W.K., Yesu Kristo aliwaambia wanafunzi wake hivi: “Mwonapo mara hiyo kitu chenye kuchukiza sana ambacho husababisha ukiwa, kama kilivyosemwa kupitia Danieli nabii, kikiwa kimesimama katika mahali patakatifu, . . . ndipo waacheni wale walio katika Yudea waanze kukimbilia milimani.” (Mathayo 24:15, 16) Akinukuu Danieli 11:31, Yesu aliwaonya wafuasi wake juu ya ‘kitu chenye kuchukiza sana kinachosababisha ukiwa’ cha wakati ujao. Unabii huo unaohusu mfalme wa kaskazini ulitolewa miaka 195 hivi baada ya kifo cha Antiochus wa Nne, mfalme wa mwisho wa Siria aliyekuwa mfalme wa kaskazini. Bila shaka, utawala mwingine ungekuwa mfalme wa kaskazini. Nani huyo?
5. Ni nani aliyesimama akiwa mfalme wa kaskazini, na kuchukua wadhifa uliokuwa wa Antiochus wa Nne wakati mmoja?
5 Malaika wa Yehova Mungu alitabiri hivi: “Badala yake [Antiochus wa Nne] atasimama mmoja, atakayepitisha mwenye kutoza ushuru kati ya utukufu wa ufalme wake; lakini katika muda wa siku chache ataangamizwa, si kwa hasira, wala si katika vita.” (Danieli 11:20) ‘Asimamaye’ hivyo alithibitika kuwa maliki wa kwanza wa Roma, Octavian, aliyeitwa Kaisari Augusto.—Ona “Mmoja Aheshimiwa, Yule Mwingine Adharauliwa,” kwenye ukurasa wa 248.
6. (a) ‘Mtoza-ushuru alipitishwa’ lini katika “utukufu wa ufalme,” na hilo lilikuwa na umaana gani? (b) Kwa nini twaweza kusema kwamba Augusto alikufa “si kwa hasira, wala si katika vita”? (c) Mfalme wa kaskazini alibadilika akawa nani?
6 ‘Ufalme wenye utukufu’ wa Augusto ulitia ndani “nchi ya uzuri”—Yudea, mkoa wa Roma. (Danieli 11:16) Mwaka wa 2 K.W.K., Augusto alimtuma ‘mtoza-ushuru’ kwa kuagiza uandikishaji, au kuhesabiwa kwa watu, huenda ili apate kujua idadi ya watu kwa minajili ya kutoza kodi na kuwaandikisha kwa lazima kwenye utumishi wa kijeshi. Kwa sababu ya agizo hilo, Yosefu na Maria walisafiri hadi Bethlehemu wakajiandikishe, kisha Yesu akazaliwa mahali palipotabiriwa. (Mika 5:2; Mathayo 2:1-12) Agosti mwaka wa 14 W.K.—“katika muda wa siku chache,” au punde baada ya kuagiza uandikishaji—Augusto akafa akiwa na umri wa miaka 76, si “kwa hasira” mikononi mwa muuaji wala “katika vita,” bali kwa sababu ya ugonjwa. Kwa kweli, mfalme wa kaskazini alikuwa amebadilika! Kufikia sasa mfalme huyo alikuwa Milki ya Roma ikiwa na watawala wake.
‘MWENYE KUDHARAULIWA ASIMAMA’
7, 8. (a) Ni nani aliyechukua mahali pa Augusto akiwa mfalme wa kaskazini? (b) Kwa nini Kaisari Augusto alimpa mwandamizi wake “heshima ya ufalme” kwa shingo upande?
7 Akiendelea na unabii huo, malaika asema hivi: “Badala yake [Augusto] atasimama mmoja, mtu astahiliye kudharauliwa, ambaye hawakumpa heshima ya ufalme; naye atakuja wakati wa amani, naye ataupata ufalme kwa kujipendekeza [“kunyakua ufalme kwa hila,” BHN]. Na wale wenye silaha mfano wa gharika watagharikishwa mbele yake, na kuvunjika; naam, mkuu wa maagano pia.”—Danieli 11:21, 22.
8 “Mtu astahiliye kudharauliwa” alikuwa Kaisari Tiberio, mwana wa Livia, mke wa tatu wa Augusto. (Ona “Mmoja Aheshimiwa, Yule Mwingine Adharauliwa,” kwenye ukurasa wa 248.) Augusto alimchukia mwana wake wa kambo kwa sababu ya tabia yake mbaya wala hakutaka awe Kaisari baada yake. Alimpa “heshima ya ufalme” shingo upande baada ya watu wote ambao wangeweza kuwa Kaisari kufa. Augusto alimwasilisha Tiberio mwaka wa 4 W.K. na kumfanya awe mrithi wa ufalme. Baada ya Augusto kufa, Tiberio mwenye umri wa miaka 54—mwenye kudharauliwa—‘akasimama,’ akitwaa mamlaka ya kuwa maliki wa Roma na mfalme wa kaskazini.
9. Tiberio ‘alinyakuaje ufalme kwa hila’?
9 “Tiberio,” yasema The New Encyclopædia Britannica, “alitumia hila dhidi ya Seneti wala hakuiruhusu imteue awe maliki kwa zaidi ya mwezi mmoja [baada ya Augusto kufa].” Aliiambia Seneti kwamba hakuna mtu yeyote ila Augusto aliyekuwa na uwezo wa kubeba mzigo wa kutawala Milki ya Roma na akawaomba maseneta waweke kikundi cha watu kimiliki badala ya mtu mmoja. “Bila kunuia kukubali aliyosema,” akaandika mwanahistoria Will Durant, “Seneti ilibembelezana-bembelezana naye mpaka hatimaye akaikubali mamlaka hiyo.” Durant alisema hivi pia: “Pande zote mbili zilikuwa zikijifanya. Tiberio alitaka kuwa maliki wa Roma, la sivyo angalipata njia ya kuuhepa umaliki; Seneti ilimhofu na kumchukia, lakini haikutaka tena kuwa jamhuri, kama ile ya kale, ambayo ilitegemea mabunge ya watawala ya kuwaziwa tu.” Kwa hiyo, Tiberio ‘akaunyakua ufalme kwa hila.’
10. ‘Silaha mfano wa gharika zilivunjwaje’?
10 “Na wale wenye silaha mfano wa gharika”—majeshi ya falme zilizozunguka—malaika alisema hivi: “Watagharikishwa mbele yake, na kuvunjika.” Tiberio alipokuwa mfalme wa kaskazini, mpwa wake wa kiume Kaisari Germanicus alikuwa kamanda wa vikosi vya Roma kwenye Mto Rhine. Mwaka wa 15 W.K., Germanicus aliongoza majeshi yake dhidi ya shujaa Mjerumani Arminius, naye akafaulu kwa kiasi fulani. Hata hivyo, ushindi huo ulimgharimu sana, naye Tiberio akaacha mambo ya Ujerumani. Badala yake, kwa kuendeleza vita vya kikabila, alijaribu kuyazuia makabila ya Ujerumani yasiungane. Kwa kawaida, Tiberio alipendelea sera ya kujikinga na nchi za kigeni naye akakazia fikira kuimarisha mipaka. Sera hiyo ya kujikinga ilikuwa na mafanikio kwa kiasi fulani. Kwa njia hiyo “silaha mfano wa gharika” zikadhibitiwa na ‘kuvunjwa.’
11. ‘Mkuu wa maagano alivunjwaje’?
11 “Mkuu wa maagano” ambayo Yehova Mungu alikuwa amefanya na Abrahamu ili kubariki familia zote duniani ‘alivunjwa’ pia. Yesu Kristo alikuwa Mbegu ya Abrahamu iliyoahidiwa katika agano hilo. (Mwanzo 22:18; Wagalatia 3:16) Nisani 14, 33 W.K., Yesu alisimama mbele ya Pontio Pilato katika jumba la gavana wa Roma huko Yerusalemu. Makuhani Wayahudi walikuwa wamemshtaki Yesu kuwa mhaini dhidi ya maliki. Lakini Yesu alimwambia Pilato hivi: “Ufalme wangu si sehemu ya ulimwengu huu. . . . Ufalme wangu si kutoka chanzo hiki.” Kwa kuwa Wayahudi hawakutaka gavana Mroma amwachilie Yesu asiye na hatia, walipaaza sauti, wakisema: “Ukimfungua mtu huyu, wewe si rafiki ya Kaisari. Kila mtu anayejifanya mwenyewe mfalme asema vibaya dhidi ya Kaisari.” Baada ya kuagiza Yesu auawe, walisema hivi: “Sisi hatuna mfalme ila Kaisari.” Kulingana na sheria ya ‘uhaini,’ ambayo Tiberio alikuwa ameipanua itie ndani kumtukana Kaisari kwa njia yoyote, Pilato akamtoa Yesu ‘avunjwe,’ au atundikwe kwenye mti wa mateso.—Yohana 18:36; 19:12-16; Marko 15:14-20.
MKANDAMIZAJI ‘ATUNGA HILA ZAKE’
12. (a) Ni nani waliofanya maagano na Tiberio? (b) Tiberio ‘alikuwaje hodari pamoja na watu wadogo’?
12 Bado akitoa unabii juu ya Tiberio, malaika alisema hivi: “Na baada ya maagano atatenda kwa hila; maana atapanda, naye atakuwa hodari pamoja na watu wadogo.” (Danieli 11:23) Washiriki wa Seneti ya Roma walikuwa ‘wamefanya maagano’ ya kikatiba na Tiberio, naye aliwategemea kihalali. Lakini alitenda kwa hila, hata akawa “hodari pamoja na watu wadogo.” Watu hao wadogo walikuwa Walindaji wa Praetori wa Roma waliokuwa wamepiga kambi karibu na kuta za Roma. Ukaribu huo uliogofya Seneti na kumsaidia Tiberio adhibiti maasi yoyote dhidi ya mamlaka yake miongoni mwa watu wa kawaida. Tiberio aliendelea kuwa mwenye nguvu akitumia walinzi 10,000.
13. Tiberio alishindaje baba zake?
13 Malaika huyo aliongeza kusema hivi kiunabii: “Wakati wa amani atapaingia mahali palipofanikiwa sana pa wilaya hiyo; naye atatenda mambo ambayo baba zake hawakuyatenda, wala babu zake; atatawanya kati yao mawindo, na mateka, na mali; naam, atatunga hila zake juu ya ngome, hata wakati ulioamriwa.” (Danieli 11:24) Tiberio alikuwa mwenye kushukushuku sana, naye aliagiza watu wengi wauawe alipokuwa akitawala. Hasa kwa sababu ya Sejanus, kamanda wa Walindaji wa Praetori, sehemu ya mwisho ya utawala wake iliogofya sana. Hatimaye, Sejanus mwenyewe akaanza kushukiwa kisha akauawa. Tiberio alishinda baba zake katika kuwakandamiza watu.
14. (a) Tiberio alitawanyaje “mawindo, na mateka, na mali” kotekote katika mikoa ya Roma? (b) Watu walimwonaje Tiberio kufikia wakati alipokufa?
14 Hata hivyo, Tiberio alitawanya “mawindo, na mateka, na mali” kotekote katika mikoa ya Roma. Alipokufa, raia zake wote walikuwa na ufanisi. Kodi hazikuwa zenye kulemea, naye alikuwa mkarimu kwa wale waliokuwa na magumu. Iwapo askari au maofisa walimwonea yeyote au kuendeleza mambo yasiyo ya kawaida katika kushughulikia mambo, wangaliweza kutarajia kisasi cha mtawala. Kuwa na mamlaka imara kulidumisha usalama, na mfumo ulioboreshwa wa kuwasiliana ulisaidia katika biashara. Tiberio alihakikisha kwamba mambo yalifanywa bila upendeleo na kwa utaratibu ndani na nje ya Roma. Kuendeleza mabadiliko yaliyoanzishwa na Kaisari Augusto kuliboresha sheria, na mifumo ya kijamii na ya kiadili. Hata hivyo, Tiberio ‘alitunga hila zake,’ hivi kwamba mwanahistoria Mroma Tasito alimfafanua kuwa mnafiki, mwenye ustadi wa kujifanya. Kufikia wakati alipokufa Machi 37 W.K., Tiberio alionwa kuwa mkandamizaji.
15. Roma iliendeleaje mwishoni mwa karne ya kwanza na mwanzoni mwa karne ya pili W.K.?
15 Wamaliki waliotawala baada ya Tiberio ambao walikuwa wafalme wa kaskazini walitia ndani Kaisari Gayo (Caligula), Klaudio wa Kwanza, Nero, Vaspasiani, Tito, Domitiani, Nerva, Trajani, na Hadriani. “Kwa muda mrefu,” chasema kichapo The New Encyclopædia Britannica, “wamaliki waliotawala baada ya Augusto waliendeleza sera zake za kutawala na miradi yake ya ujenzi, ingawa hawakuanzisha mambo mengi nao walikuwa wenye kujionyesha sana.” Kichapo hichohicho chataarifu hivi: “Mwishoni mwa karne ya 1 na mwanzoni mwa karne ya 2, Roma ilikuwa imefikia upeo wa utukufu nayo ilikuwa na wakazi wengi zaidi.” Ingawa Roma ilikuwa na matatizo kadhaa kwenye mipaka yake, pambano lake la kwanza lililotabiriwa dhidi ya mfalme wa kusini halikutukia hadi karne ya tatu W.K.
ACHOCHEWA DHIDI YA MFALME WA KUSINI
16, 17. (a) Ni nani aliyekuwa mfalme wa kaskazini anayetajwa kwenye Danieli 11:25? (b) Ni nani aliyekuja kuwa mfalme wa kusini, na hilo lilitukiaje?
16 Malaika wa Mungu aliendelea na unabii huo, akisema hivi: “Naye [mfalme wa kaskazini] atachochea nguvu zake na ushujaa wake juu ya huyo mfalme wa kusini kwa jeshi kubwa; na mfalme wa kusini atafanya vita kwa jeshi kubwa mno lenye nguvu nyingi; lakini [mfalme wa kaskazini] hatasimama; maana watatunga hila juu yake. Naam, walao sehemu ya chakula chake watamwangamiza, na jeshi lake litagharikishwa; na wengi wataanguka wameuawa.”—Danieli 11:25, 26.
17 Miaka 300 hivi baada ya Octavian kufanya Misri iwe mkoa wa Roma, Maliki Mroma Aurelian akawa mfalme wa kaskazini. Wakati huohuo, Malkia Septimia Zenobia wa koloni ya Roma ya Palmyra akawa mfalme wa kusini.a (Ona “Zenobia—Malkia Mpiganaji wa Palmyra,” kwenye ukurasa wa 252.) Jeshi la Palmyra lilikuwa likimiliki Misri mwaka wa 269 W.K. likisingizia kuwa lilikuwa likiifanya iwe salama kwa ajili ya Roma. Zenobia alitaka kufanya Palmyra liwe jiji kuu huko mashariki na alitaka kutawala mikoa ya mashariki ya Roma. Akishtuliwa na tamaa ya makuu ya Zenobia, Aurelian alichochea “nguvu zake na ushujaa wake” dhidi ya Zenobia.
18. Matokeo ya pambano kati ya Maliki Aurelian, mfalme wa kaskazini, na Malkia Zenobia, mfalme wa kusini yalikuwa nini?
18 Mfalme wa kusini, yaani serikali ya Zenobia, ‘alifanya’ vita dhidi ya mfalme wa kaskazini “kwa jeshi kubwa mno lenye nguvu nyingi” chini ya majenerali wawili, Zabdas na Zabbai. Lakini Aurelian aliteka Misri kisha akafunga safari kwenda Asia Ndogo na Siria. Zenobia alishindwa huko Emesa (kuitwako Homs leo), akakimbia na kwenda Palmyra. Aurelian alipolizingira jiji hilo, Zenobia alilipigania kufa na kupona lakini hakufanikiwa. Yeye na mwanaye wakakimbia kuelekea Uajemi, wakakamatwa na Waroma kwenye Mto Eufrati. Watu wa Palmyra walisalimisha jiji lao mwaka wa 272 W.K. Aurelian hakumuua Zenobia, hilo likimfanya avutie watu wengi katika ule msafara wa ushindi kupitia Roma mwaka 274 W.K. Aliishi maisha yake yaliyosalia akiwa mke Mroma.
19. Aurelian aliangukaje kwa sababu ya ‘hila zilizotungwa juu yake’?
19 Aurelian mwenyewe ‘hakusimama kwa sababu ya hila zilizotungwa juu yake.’ Mwaka wa 275 W.K., alifunga safari kwenda kupigana na Waajemi. Alipokuwa akingoja huko Thrasi ili apate fursa ya kuvuka mlango-bahari na kuingia Asia Ndogo, wale ‘waliokula sehemu ya chakula chake’ walitunga hila juu yake na ‘kumwangamiza.’ Alinuia kumwadhibu mwandishi wake Eros kwa sababu mambo hayakuwa shwari. Hata hivyo, Eros akaandika orodha bandia ya majina ya maofisa kadhaa waliotiwa alama wauawe. Maofisa hao walipoiona orodha hiyo walipanga njama na kumwua Aurelian.
20. “Jeshi” la mfalme wa kaskazini ‘liligharikishwaje’?
20 Mfalme wa kaskazini hakutoweka Maliki Aurelian alipokufa. Waroma wengine walitawala baada yake. Kwa muda fulani kulikuwa na maliki wa magharibi na maliki wa mashariki. Chini yao “jeshi” la mfalme wa kaskazini ‘liligharikishwa,’ au ‘kutawanywa,’b na wengi ‘walianguka wameuawa’ kwa sababu ya uvamizi wa makabila ya Kijerumani kutoka kaskazini. Wagothi walivuka mipaka ya Roma katika karne ya nne W.K. Uvamizi uliendelea, mmoja baada ya mwingine. Mwaka wa 476 W.K., kiongozi wa Ujerumani, Odoacer alimwondoa maliki wa mwisho aliyekuwa akitawala Roma. Kufikia mwanzoni mwa karne ya sita, Milki ya Roma ya upande wa magharibi ilikuwa imevunjwa-vunjwa, na wafalme Wajerumani walikuwa wakitawala Afrika Kaskazini, Gaul, Hispania, Italia, na Uingereza. Upande wa mashariki wa milki hiyo ulidumu hadi karne ya 15.
MILKI KUBWA YAGAWANYIKA
21, 22. Konstantino alitokeza mabadiliko gani katika karne ya nne W.K.?
21 Malaika wa Yehova aliendelea kutabiri uporaji zaidi wa mfalme wa kaskazini na mfalme wa kusini bila kutaja mambo madogo-madogo yasiyohitajika juu ya kuvunjika kwa Milki ya Roma. Hata hivyo, kupitia kifupi mambo fulani yaliyotukia katika Milki ya Roma kutatusaidia kuwatambua wafalme hao wawili wakati ujao.
22 Katika karne ya nne, Maliki Mroma Konstantino alifanya Serikali iutambue Ukristo uliokuwa umeasi. Hata aliitisha na kusimamia baraza la kanisa huko Nisea, Asia Ndogo, mwaka wa 325 W.K. Baadaye, Konstantino alihamisha makao ya kifalme kutoka Roma hadi Byzantium, au Constantinople, akilifanya jiji hilo jipya kuwa jiji lake kuu. Milki ya Roma iliendelea chini ya utawala wa maliki mmoja hadi Maliki Theodosius wa Kwanza alipokufa Januari 17, 395 W.K.
23. (a) Milki ya Roma iligawanyikaje Theodosius alipokufa? (b) Milki ya Mashariki ilikoma lini? (c) Ni nani aliyetawala Misri kufikia mwaka wa 1517?
23 Theodosius alipokufa, wana wake waligawanya Milki ya Roma miongoni mwao. Honorius alipokea sehemu ya magharibi, naye Arcadius akapokea mashariki, Constantinople likiwa jiji lake kuu. Afrika Kaskazini, Gaul, Hispania, Italia, na Uingereza ilikuwa baadhi ya mikoa ya milki ya magharibi. Makedonia, Thrasi, Asia Ndogo, Siria, na Misri ilikuwa mikoa ya milki ya mashariki. Mwaka wa 642 W.K., Aleksandria, jiji kuu la Misri, lilianguka mikononi mwa Waarabu, na Misri ikawa mkoa wa makhalifa. Katika Januari 1449, Konstantino wa 11 akawa maliki wa mwisho wa mashariki. Waturuki wakiongozwa na Sultan Mehmed wa Pili waliteka Constantinople Mei 29, 1453, na kuikomesha Milki ya Roma Mashariki. Misri ikawa mkoa wa Uturuki mwaka wa 1517. Hata hivyo, hatimaye nchi hiyo ya mfalme wa kale wa kusini ingetawalwa na milki nyingine kutoka magharibi.
24, 25. (a) Kulingana na wanahistoria fulani, ni nini kilichoonyesha mwanzo wa Milki Takatifu ya Roma? (b) Ni nini kilichotokea hatimaye kwa lile jina la cheo “maliki” la Milki Takatifu ya Roma?
24 Askofu Mkatoliki wa Roma, aitwaye Papa Leo wa Kwanza, aliyekuwa maarufu kwa kusisitiza mamlaka ya papa katika karne ya tano W.K., alizuka upande wa magharibi wa Milki ya Roma. Hatimaye, papa huyo akajiamulia kumtawaza maliki wa upande wa magharibi. Ilitukia hivyo huko Roma kwenye Krismasi ya mwaka wa 800 W.K., Papa Leo wa Tatu alipomtawaza Mfalme Charles (Charlemagne) wa Wafaranka awe maliki wa Milki mpya ya Roma Magharibi. Kutawaza huko kulianzisha tena umaliki huko Roma na, kulingana na wanahistoria fulani, kulionyesha mwanzo wa Milki Takatifu ya Roma. Tangu wakati huo na kuendelea kulikuwa na Milki ya Mashariki na Milki Takatifu ya Roma iliyokuwa magharibi, milki zote mbili zikidai kuwa za Kikristo.
25 Kadiri wakati ulivyopita, waliotawala baada ya Charlemagne hawakuwa na matokeo yoyote. Hata kwa muda fulani hakukuwa na maliki. Wakati huohuo, Mfalme wa Ujerumani Otto wa Kwanza alikuwa ameanza kutawala sehemu kubwa ya kaskazini na ya kati ya Italia. Akajitangaza kuwa mfalme wa Italia. Februari 2, 962 W.K., Papa John wa 12 alimtawaza Otto wa Kwanza kuwa maliki wa Milki Takatifu ya Roma. Jiji lake kuu lilikuwa Ujerumani, nao wamaliki walikuwa Wajerumani, kama vile wengi wa raia zake walivyokuwa Wajerumani. Karne tano baadaye, watawala wa Kijerumani waliotawala Austria waliitwa “maliki,” nao waliendelea kuitwa hivyo kwa muda mrefu katika ile miaka iliyosalia ya Milki Takatifu ya Roma.
WALE WAFALME WAWILI WATAMBULIKA WAZIWAZI TENA
26. (a) Ni nini kiwezacho kusemwa juu ya mwisho wa Milki Takatifu ya Roma? (b) Ni nani aliyetokea akiwa mfalme wa kaskazini?
26 Napoléon wa Kwanza aliipiga na kuiangamiza Milki Takatifu ya Roma alipokataa kutambua kuwepo kwa milki hiyo baada ya ushindi wake mbalimbali huko Ujerumani mwaka wa 1805. Kwa kuwa alishindwa kuitetea taji, Maliki Francis wa Pili alijiuzulu kutoka katika utawala wa Roma Agosti 6, 1806, na kurudia serikali yake ya kitaifa akiwa maliki wa Austria. Baada ya miaka 1,006, ile Milki Takatifu ya Roma—iliyoanzishwa na Leo wa Tatu, papa Mkatoliki, na Charlemagne, mfalme Mfaranka—ikakoma. Mwaka wa 1870, Roma likawa jiji kuu la ufame wa Italia, usiotegemea Vatikani. Mwaka uliofuata, milki ya Kijerumani ikaanza, Wilhelm wa Kwanza akateuliwa kuwa kaisari. Kwa hiyo, mfalme wa kaskazini wa kisasa—Ujerumani—akatokea duniani.
27. (a) Misri ilipataje kuwa chini ya himaya ya Uingereza? (b) Ni nani aliyepata kuwa mfalme wa kusini?
27 Lakini mfalme wa kusini wa kisasa alikuwa nani? Historia yaonyesha kwamba Uingereza ilitwaa mamlaka katika karne ya 17. Akinuia kukatisha njia za kibiashara za Uingereza, Napoléon wa Kwanza alishinda Misri mwaka wa 1798. Vita vikazuka, na muungano wa Waingereza na Waturuki ukawaondolea mbali Wafaransa kutoka Misri, ambayo mwanzoni, ilitambulishwa kuwa mfalme wa kusini. Katika karne iliyofuata, uvutano wa Uingereza huko Misri uliongezeka. Baada ya mwaka wa 1882, Misri ilikuwa ikitegemea Uingereza hasa. Vita ya Ulimwengu ya Kwanza ilipozuka mwaka wa 1914, Misri ilimilikiwa na Uturuki nayo ilitawalwa na gavana. Hata hivyo, baada ya Uturuki kujiunga na Ujerumani katika vita hiyo, Uingereza ilimwondoa gavana huyo na kuitangaza Misri kuwa chini ya himaya ya Uingereza. Uingereza na Marekani zilianza kuwa na uhusiano wa karibu hatua kwa hatua na hatimaye zikawa Serikali ya Ulimwengu ya Uingereza na Marekani. Zikiwa pamoja zikawa mfalme wa kusini.
[Maelezo ya Chini]
a Kwa kuwa majina “mfalme wa kaskazini” na “mfalme wa kusini” ni majina ya cheo, yaweza kurejezea chochote chenye kutawala, kutia ndani mfalme, malkia, au mataifa kadhaa yakiwa pamoja.
b Ona kielezi-chini kwenye Danieli 11:26 katika New World Translation of the Holy Scriptures—With References, iliyochapishwa na Watchtower Bible and Tract Society of New York, Inc.
UMEFAHAMU NINI?
• Ni maliki gani wa Roma aliyekuwa wa kwanza kuwa mfalme wa kaskazini, naye alimtuma ‘mtoza-ushuru’ lini?
• Ni nani aliyekuwa mfalme wa kaskazini baada ya Augusto, naye ‘Mkuu wa maagano alivunjikaje’?
• Pambano kati ya Aurelian akiwa mfalme wa kaskazini na Zenobia akiwa mfalme wa kusini lilikuwa na matokeo gani?
• Milki ya Roma ilipatwa na nini, na ni serikali gani zilizokuwa wale wafalme wawili kufikia mwisho wa karne ya 19?
[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 248-251]
MMOJA AHESHIMIWA, YULE MWINGINE ADHARAULIWA
MMOJA alibadili jamhuri iliyojaa zogo ikawa milki ya ulimwengu. Yule mwingine akaongeza utajiri wa milki hiyo mara 20 katika miaka 23. Mmoja aliheshimiwa alipokufa, ilhali yule mwingine alidharauliwa. Maliki hao wawili walitawala Roma wakati wa maisha na huduma ya Yesu. Walikuwa nani? Na kwa nini mmoja wao akaheshimiwa, hali yule mwingine hakuheshimiwa?
‘ALIKUTA ROMA IKIWA MATUFALI AKAIACHA IKIWA MARUMARU’
Mwaka wa 44 K.W.K., Kaisari Yulio alipouawa, mjukuu wa dada yake, Gayo Octavian alikuwa na umri wa miaka 18 tu. Kwa kuwa alikuwa mwana wa kambo wa Kaisari Yulio na mrithi wake mkuu, Octavian mchanga alifunga safari mara moja kuelekea Roma akadai urithi wake. Huko alikutana na mpinzani mgumu—ofisa mkuu wa Kaisari, Mark Antony, aliyetarajia kuwa mrithi mkuu. Kisha kukawa na mgogoro wa kisiasa na kung’ang’ania mamlaka kwa muda wa miaka 13.
Octavian aliibuka akiwa mtawala wa Milki ya Roma asiyepingwa alipoyashinda majeshi ya muungano ya Malkia Kleopatra wa Misri na mpenzi wake Mark Antony (mwaka wa 31 K.W.K.). Mwaka uliofuata Antony na Kleopatra wakajiua, naye Octavian akatwaa Misri. Kwa hiyo, masalio ya Milki ya Ugiriki yakaondolewa kabisa, na Roma ikawa serikali ya ulimwengu.
Octavian alikuwa mwangalifu asirudie makosa ya Kaisari Yulio kwa kuwa alikumbuka kwamba Yulio aliuawa kwa sababu ya udhalimu wake. Ili asikiuke maoni ya Waroma ya kupendelea jamhuri, aliufanya utawala wake uonekane kana kwamba ulikuwa jamhuri. Alikataa kuitwa “mfalme” na “dikteta.” Isitoshe, alijulisha wazi kwamba alinuia kuipatia Seneti ya Roma mikoa yote iitawale na kwamba alikuwa tayari kujiuzulu kutoka katika wadhifa wake. Mbinu hiyo ilifanikiwa. Seneti yenye uthamini ilimsihi sana Octavian aendelee katika wadhifa wake na aendelee kutawala baadhi ya mikoa.
Tena, Januari 16, 27 K.W.K., Seneti ilimpa Octavian cheo “Augusto,” kinachomaanisha “Aliyekwezwa, Mtakatifu.” Octavian alikubali cheo hicho na pia akauita mwezi mmoja kutokana na jina lake na kuazima siku moja kutoka katika mwezi wa Februari ili mwezi wa Agosti uwe na siku zinazotoshana na zile za mwezi wa Julai, mwezi uliopata jina kutokana na Kaisari Yulio. Octavian akawa maliki wa kwanza wa Roma na baadaye akaja kuitwa Kaisari Augusto, au “Mwadhamu.” Baadaye akaitwa “pontifex maximus” (kuhani wa cheo cha juu), na mwaka wa 2 K.W.K.—mwaka aliozaliwa Yesu—Seneti ikamwita Pater Patriae, “Baba wa Nchi Yake.”
Mwaka huohuo, “agizo kutoka kwa Kaisari Augusto likatoka kwamba dunia yote inayokaliwa ipate kusajiliwa; . . . na watu wote wakaanza kusafiri kwenda kusajiliwa, kila mmoja kwenye jiji lake mwenyewe.” (Luka 2:1-3) Kwa sababu ya agizo hilo, Yesu alizaliwa Bethlehemu kulingana na unabii wa Biblia.—Danieli 11:20; Mika 5:2.
Serikali ya Augusto ilifuatia haki na ilikuwa na uchumi bora. Augusto alitokeza mfumo wa posta wenye matokeo, akajenga barabara na madaraja. Alipanga upya jeshi, akaunda jeshi la majini lenye kudumu, na kikundi cha mashujaa cha walinzi wa maliki walioitwa Walindaji wa Praetori. (Wafilipi 1:13) Chini ya utawala wake waandikaji kama Virgil na Horace walisitawi na wachongaji walichonga vinyago maridadi ambavyo leo huitwa mtindo bora wa kale. Augusto alimalizia kujenga majengo ambayo Kaisari Yulio hakumaliza na akajenga upya mahekalu mengi. Ile Pax Romana (“Amani ya Roma”) aliyoanzisha ilidumu kwa zaidi ya miaka 200. Augusto alikufa Agosti 19, 14 W.K., akiwa na umri wa miaka 76 naye akawa akiabudiwa kama mungu.
Augusto alijisifu kwamba ‘alikuta Roma ikiwa matufali na akaiacha ikiwa marumaru.’ Kwa kuwa hakutaka Roma irejelee siku za awali zilizojaa zogo za jamhuri iliyotangulia, alinuia kumtayarisha maliki ambaye angefuata. Lakini hakuwa na watu wengi wa kuchagua. Mpwa wake wa kiume, wajukuu wake wawili, mwana-mkwe, na mwana mmoja wa kambo, wote hao walikuwa wamekufa, na kumwacha Tiberio aliyekuwa mwana wa kambo peke yake atwae umaliki.
“ASTAHILIYE KUDHARAULIWA”
Haukupita mwezi mmoja baada ya Augusto kufa, Seneti ya Roma ikamteua Tiberio aliyekuwa na umri wa miaka 54 awe maliki. Tiberio aliishi na kutawala hadi Machi 37 W.K. Kwa hiyo, alikuwa maliki wa Roma wakati wa huduma ya Yesu ya hadharani.
Akiwa maliki, Tiberio alikuwa na sifa nzuri na sifa mbaya. Mojawapo ya sifa zake nzuri ni kwamba hakutumia fedha ovyoovyo kwa ajili ya anasa. Kwa sababu hiyo, milki yake ilisitawi naye alikuwa na fedha za kusaidia kukabiliana na misiba na nyakati mbaya. Tiberio alijiona mwenyewe kuwa mwanadamu tu, alikataa vyeo vingi vyenye kuheshimika, na kwa kawaida alielekeza ibada ya maliki kwa Augusto badala yake mwenyewe. Hakuupatia mwezi wa kalenda jina kutokana na jina lake mwenyewe kama vile Augusto na Kaisari Yulio walivyokuwa wamefanya, wala hakuwaruhusu wengine wamheshimu kwa njia hiyo.
Hata hivyo, sifa mbaya za Tiberio zilizidi sifa zake nzuri. Alikuwa mwenye kushuku sana na mwenye unafiki alipokuwa akishughulika na wengine, naye aliagiza watu wengi wauawe alipokuwa akitawala—wengi wa waliokuwa rafiki zake awali waliuawa pia. Aliibadili sheria ya lèse-majesté (uhaini) itie ndani, makufuru dhidi yake mwenyewe, zaidi ya matendo ya uchochezi. Yadhaniwa kwamba Wayahudi walimsonga Gavana Mroma Pontio Pilato aagize Yesu auawe kwa kutegemea nguvu za sheria hiyo.—Yohana 19:12-16.
Tiberio aliweka Walindaji wengi wa Praetori karibu na Roma kwa kujenga kambi zenye ngome kaskazini mwa kuta za jiji hilo. Kuwepo kwa Walindaji hao kuliogofya Seneti ya Roma, iliyokuwa ikitisha mamlaka yake, na pia kulidhibiti maasi yoyote miongoni mwa watu. Tiberio pia alitia moyo mfumo wa kushtakiana, na kipindi cha mwisho cha utawala wake kilikuwa chenye kuogofya.
Kufikia wakati wa kifo chake, Tiberio alionwa kuwa mkandamizaji. Alipokufa, Waroma walishangilia nayo Seneti ikakataa kumfanya awe mungu. Kwa sababu hiyo na nyinginezo, twaona Tiberio alitimiza unabii unaosema kwamba “astahiliye kudharauliwa” angeinuka akiwa “mfalme wa kaskazini.”—Danieli 11:15, 21.
UMEFAHAMU NINI?
• Octavian alipataje kuwa maliki wa kwanza wa Roma?
• Twaweza kusema nini juu ya mafanikio ya Serikali ya Augusto?
• Tiberio alikuwa na sifa gani nzuri na mbaya?
• Tiberio alitimizaje unabii juu ya astahiliye kudharauliwa?
[Picha]
Tiberio
[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 252-252]]
ZENOBIA—MALKIA MPIGANAJI WA PALMYRA
“ALIKUWA mweusi-mweusi . . . Meno yake yalikuwa meupe kama lulu, na macho yake makubwa meusi yaling’aa kama moto usio wa kawaida, nayo yalivutia sana. Sauti yake ilikuwa yenye nguvu na tamu. Kujifunza kuliimarisha na kuboresha uelewevu wake wa kiume. Alijua Kilatini, na alijua vizuri Kigiriki, Kiaramu, na lugha za Misri.” Ndivyo mwanahistoria Edward Gibbon alivyomsifu Zenobia—malkia mpiganaji wa Palmyra, jiji la Siria.
Mume wa Zenobia ndiye Odaenathus, kabaila Mpalmyra, aliyetunukiwa wadhifa wa balozi wa Roma mwaka wa 258 W.K. kwa sababu alikuwa amefanikiwa katika vita dhidi ya Uajemi kwa niaba ya Milki ya Roma. Miaka miwili baadaye, Odaenathus alipokea kutoka kwa Maliki Gallienus wa Roma cheo cha corrector totius Orientis (gavana wa Mashariki yote). Hiyo ilikuwa kwa sababu alimshinda Mfalme wa Uajemi, Shāpūr wa Kwanza. Hatimaye Odaenathus akajiita “mfalme wa wafalme.” Huenda kwa kiasi kikubwa Odaenathus alipata ushindi mbalimbali kwa sababu ya ujasiri na busara ya Zenobia.
ZENOBIA ATAMANI KUJENGA MILKI
Mwaka wa 267 W.K., akiwa katika upeo wa ufanisi wake, Odaenathus na mrithi wake waliuawa. Zenobia akatwaa wadhifa wa mume wake kwa kuwa mwana wake alikuwa mchanga sana asiweze kuutwaa. Kwa kuwa alikuwa mrembo, mwenye kutamani makubwa, msimamizi mwenye uwezo, aliyezoea kupiga vita akiwa na mumewe, na mfasaha wa lugha kadhaa, alistahiwa na kuungwa mkono na raia zake. Zenobia alipenda kujifunza naye alishirikiana na watu wengi wenye akili. Mmoja wa washauri wake alikuwa mwanafalsafa na pia mwalimu wa ufasaha wa kusema aitwaye Cassius Longinus—yasemekana alikuwa na ‘ujuzi mwingi.’ Katika kitabu Palmyra and Its Empire—Zenobia’s Revolt Against Rome, mwandikaji Richard Stoneman aandika hivi: “Miaka mitano baada ya Odenathus kufa . . . , Zenobia alikuwa amejiimarisha akilini mwa watu wake kuwa bibi wa Mashariki.”
Uajemi ilikuwa upande mmoja wa milki ya Zenobia, ambayo yeye na mume wake walikuwa wameidhoofisha, nayo Roma iliyokuwa ikianguka ilikuwa upande wa pili. Kuhusu hali katika Milki ya Roma wakati huo, mwanahistoria J. M. Roberts asema hivi: “Karne ya tatu ilikuwa . . . wakati mbaya kwa Roma kwenye mipaka ya mashariki hali kadhalika mipaka ya magharibi, ilhali nyumbani kipindi kipya cha vita vya wenyewe kwa wenyewe na ubishi juu ya waandamizi ulikuwa umeanza. Maliki ishirini na wawili (bila kuhesabu waliojisingizia kuwa maliki) walitawala wakifuatana.” Naye bibi huyo wa Siria, alikuwa mtawala kamili aliyejiimarisha katika milki yake. “Akitawala mabaki ya milki mbili [Uajemi na Roma],” ataarifu Stoneman, “angeweza kutamani kujenga milki ya tatu ambayo ingezitawala zote mbili.”
Zenobia alipata fursa ya kuongeza nguvu zake za kifalme mwaka wa 269 W.K. wakati ambapo mtu aliyejisingizia kuwa mtawala na ambaye alikuwa akipinga utawala wa Roma alitokea huko Misri. Jeshi la Zenobia lilienda Misri upesi, likamwondolea mbali mwasi huyo na kutwaa nchi hiyo. Akijitangaza kuwa malkia wa Misri, alipiga chapa sarafu zenye jina lake mwenyewe. Ufalme wake sasa ulienea tokea mto Naili hadi mto Eufrati. Wakati huo maishani mwake ndipo Zenobia alipopata kuwa “mfalme wa kusini.”—Danieli 11:25, 26.
JIJI KUU LA ZENOBIA
Zenobia aliimarisha na kurembesha jiji lake kuu, Palmyra, kufikia kiwango cha kwamba lilikuwa miongoni mwa majiji makubwa zaidi ya ulimwengu wa Roma. Yakadiriwa kwamba ilikuwa na wakazi 150,000. Majumba makubwa ya umma, mahekalu, mabustani, nguzo, na nguzo za ukumbusho zilijaa Palmyra, jiji lililozingirwa kwa kuta ambazo yasemekana zilikuwa na mzingo wa kilometa 21. Safu ya nguzo za Korintho zenye kimo cha zaidi ya meta 15—zipatazo 1,500—zilikuwa kandokando ya barabara kuu. Sanamu na sanamu za kichwa na mabega za mashujaa na matajiri wafadhili zilijaa jijini. Mwaka wa 271 W.K., Zenobia alisimamisha sanamu yake mwenyewe na ya mume wake aliyekuwa amekufa.
Hekalu la Jua lilikuwa mojawapo ya majengo bora kabisa huko Palmyra na bila shaka wengi waliabudu humo. Huenda Zenobia mwenyewe aliabudu mungu aliyehusianishwa na mungu-jua. Hata hivyo, Siria ya karne ya tatu ilikuwa nchi yenye dini nyingi. Katika milki ya Zenobia kulikuwa na watu waliodai kuwa Wakristo, Wayahudi, na waabudu wa jua na mwezi. Alizionaje aina hizo mbalimbali za ibada? Mwandikaji Stoneman ataarifu hivi: “Mtawala mwenye hekima hatapuuza desturi zozote zionekanazo kuwafaa watu wake. . . . Ilitumainiwa kwamba . . . miungu ilikuwa imepatanishwa iunge mkono Palmyra.” Yaonekana kwamba Zenobia alivumilia dini mbalimbali.
Akiwa na utu mzuri, Zenobia alipendwa na watu wengi. Alitimiza fungu muhimu zaidi katika kuwakilisha utawala wa kisiasa uliotabiriwa katika unabii wa Danieli. Hata hivyo, utawala wake haukudumu zaidi ya miaka mitano. Maliki Mroma, Aurelian alimshinda Zenobia mwaka wa 272 W.K. na baadaye akapora Palmyra lisiweze kurekebishwa tena. Zenobia alihurumiwa. Yasemekana aliolewa na seneta Mroma na huenda akaishi maisha yake yaliyosalia akiwa amestaafu.
UMEFAHAMU NINI?
• Utu wa Zenobia umefafanuliwaje?
• Baadhi ya matendo ya Zenobia ya kijasiri yalikuwa gani?
• Zenobia alizionaje dini?
[Picha]
Malkia Zenobia akiwahutubia askari-jeshi wake
[Chati/Picha katika ukurasa wa 246]
WAFALME KATIKA DANIELI 11:20-26
Mfalme wa Mfalme wa
Kaskazini Kusini
Danieli 11:20 Augusto
Danieli 11:21-24 Tiberio
Danieli 11:25, 26 Aurelian Malkia Zenobia
Kuvunjika Milki ya Milki ya Uingereza,iliyo
kulikotabiriwa Ujerumani fuatwa na Serikali
kwa milki ya Ulimwengu
ya Roma ya Uingereza
kwatokezakwa na Marekani
[Picha]
Tiberio
[Picha]
Aurelian
[Picha]
Sanamu ndogo ya Charlemagne
[Picha]
Augusto
[Picha]
Meli ya vita ya Uingereza ya karne ya 17
[Picha katika ukurasa wa 230]
[Picha katika ukurasa wa 233]
Augusto
[Picha katika ukurasa wa 234]
Tiberio
[Picha katika ukurasa wa 235]
Kwa sababu ya amri ya Augusto, Yosefu na Maria walisafiri kwenda Bethlehemu
[Picha katika ukurasa wa 237]
Kama ilivyotabiriwa, Yesu ‘alivunjwa’ kwenye kifo
[Picha katika ukurasa wa 245]
1. Charlemagne 2. Napoléon wa Kwanza 3. Wilhelm wa Kwanza 4. Askari-jeshi Wajerumani, Vita ya Ulimwengu ya Kwanza