Matendo
18 Baada ya mambo haya aliondoka Athene na kuja Korintho. 2 Naye akakuta Myahudi fulani aitwaye jina Akila, mzaliwa wa Ponto aliyekuwa amekuja hivi karibuni kutoka Italia, na Prisila mke wake, kwa sababu ya uhakika wa kwamba Klaudio alikuwa ameagiza Wayahudi wote waondoke Roma. Kwa hiyo akawaendea 3 na kwa sababu ya kuwa wa kazi ileile akakaa nyumbani kwao, nao wakafanya kazi, kwa maana kikazi walikuwa ni watengeneza-mahema. 4 Hata hivyo, yeye alikuwa akitoa hotuba katika sinagogi kila sabato na alikuwa akishawishi Wayahudi na Wagiriki.
5 Basi, wakati Sila na Timotheo pia walipoteremka kutoka Makedonia, Paulo alianza kushughulika kwa juhudi nyingi na lile neno, akiwatolea Wayahudi ushahidi ili kuthibitisha kwamba Yesu ndiye Kristo. 6 Lakini baada ya wao kufuliza kupinga na kusema kwa maneno yenye kuudhi, akakung’uta mavazi yake na kuwaambia: “Damu yenu na iwe juu ya vichwa vyenu wenyewe. Mimi ni safi. Tangu sasa na kuendelea hakika nitaenda kwa watu wa mataifa.” 7 Basi akahama huko na kuingia katika nyumba ya mwanamume aitwaye jina Titio Yustasi, mwabudu wa Mungu, ambaye nyumba yake ilikuwa yashikana na sinagogi. 8 Lakini Krispo ofisa-msimamizi wa sinagogi akawa mwamini katika Bwana, na ndivyo na watu wote wa nyumbani mwake. Na wengi kati ya Wakorintho waliosikia wakaanza kuamini na kubatizwa. 9 Zaidi ya hayo, wakati wa usiku Bwana akamwambia Paulo kupitia ono: “Usiwe na hofu, bali fuliza kusema na usikae kimya, 10 kwa sababu mimi nipo pamoja na wewe na hakuna mtu atakayekushambulia ili kukutenda jambo baya; kwa maana nina watu wengi katika jiji hili.” 11 Kwa hiyo akakaa huko bila kuondoka kwa mwaka mmoja na miezi sita, akifundisha miongoni mwao neno la Mungu.
12 Sasa Galio alipokuwa prokonso wa Akaya, Wayahudi wakainuka kwa umoja dhidi ya Paulo na kumwongoza kwenye kiti cha hukumu, 13 wakisema: “Kinyume cha sheria mtu huyu huongoza watu kwenye sadikisho jingine katika kumwabudu Mungu.” 14 Lakini Paulo alipokuwa akitaka kufungua kinywa chake, Galio akawaambia Wayahudi: “Kama ingekuwa, kwa kweli, ni kosa fulani au tendo ovu la ulaghai, Enyi Wayahudi, ningechukuliana nanyi kwa subira nikiwa na sababu. 15 Lakini kama ni mabishano juu ya usemi na majina na sheria miongoni mwenu, nyinyi wenyewe lazima mwone hilo. Mimi sitaki kuwa hakimu wa mambo haya.” 16 Ndipo akawafukuza wao kutoka kwenye kiti cha hukumu. 17 Kwa hiyo wote wakamshika Sosthenesi ofisa-msimamizi wa sinagogi na kuanza kumpiga mbele ya kiti cha hukumu. Lakini Galio hakukubali kujihangaisha mwenyewe na mambo haya hata kidogo.
18 Hata hivyo, baada ya kukaa siku kadhaa zaidi, Paulo aliwaambia akina ndugu kwaheri naye akaendelea kusafiri kwa mashua kwenda Siria, na pamoja naye Prisila na Akila, kwa kuwa alikuwa amekatwa nywele za kichwa chake kuwa fupi katika Kenkrea, kwa maana alikuwa na nadhiri. 19 Kwa hiyo wakawasili Efeso, naye akawaacha huko; lakini yeye mwenyewe akaingia ndani ya sinagogi akajadiliana na Wayahudi kwa kutoa sababu. 20 Ijapokuwa walifuliza kumwomba abaki kwa muda mrefu zaidi, akawa hakubali 21 bali akasema kwaheri na kuwaambia: “Hakika nitarudi kwenu tena, ikiwa Yehova anapenda.” Naye akaanza kusafiri baharini kutoka Efeso 22 na kuteremka hadi Kaisaria. Naye akapanda kwenda akalisalimu kutaniko, na kuteremka kwenda Antiokia.
23 Na alipokuwa amepisha wakati fulani huko akaondoka na kwenda mahali hadi mahali kupitia nchi ya Galatia na Frigia, akiwatia nguvu wanafunzi wote.
24 Sasa Myahudi fulani aitwaye jina Apolo, mzaliwa wa Aleksandria, mwanamume mfasaha, aliwasili Efeso; naye alikuwa mwenye ujuzi mwingi katika Maandiko. 25 Mwanamume huyu alikuwa amefundishwa kwa mdomo katika njia ya Yehova na, kwa kuwa alikuwa amewaka roho, akaanza kusema na kuyafundisha kwa usahihi mambo juu ya Yesu, lakini akiwa aufahamu ubatizo wa Yohana tu. 26 Na mwanamume huyu akaanza kusema kwa ujasiri katika sinagogi. Prisila na Akila walipomsikia, walishirikiana naye na kumfafanulia kwa usahihi zaidi njia ya Mungu. 27 Zaidi, kwa sababu alikuwa akitaka kwenda kuvuka aingie Akaya, akina ndugu wakawaandikia wanafunzi, wakiwahimiza kwa bidii wampokee kwa fadhili. Kwa hiyo alipofika huko, aliwasaidia sana wale waliokuwa wameamini kwa sababu ya fadhili isiyostahiliwa [ya Mungu]; 28 kwa maana kwa juhudi nyingi alithibitisha kikamili hadharani kuwa Wayahudi ni wenye makosa, huku akionyesha kwa Maandiko kwamba Yesu alikuwa ndiye Kristo.