Ufunuo
14 Nami nikaona, na, tazama! Mwana-Kondoo amesimama juu ya Mlima Zayoni, na pamoja naye mia arobaini na nne elfu wakiwa na jina lake na jina la Baba yake limeandikwa juu ya vipaji vya nyuso zao. 2 Nami nikasikia mvumo kutoka mbinguni kama mvumo wa maji mengi na kama mvumo wa ngurumo kubwa; na mvumo niliosikia ulikuwa kama wa waimbaji ambao hufuatanisha sauti zao wenyewe na kinubi wakipiga vinubi vyao. 3 Nao wanaimba kama kwamba wimbo mpya mbele ya hicho kiti cha ufalme na mbele ya viumbe hai wanne na wazee; na hakuna yeyote aliyeweza kuwa bingwa wa ule wimbo ila mia arobaini na nne elfu, ambao wamenunuliwa kutoka katika dunia. 4 Hawa ndio wale ambao hawakujitia wenyewe unajisi na wanawake; kwa kweli, wao ni mabikira. Hawa ndio wafulizao kumfuata Mwana-Kondoo hata iwe ni wapi aendako. Hawa walinunuliwa kutoka miongoni mwa wanadamu wakiwa matunda ya kwanza kwa Mungu na kwa Mwana-Kondoo, 5 na lolote lisilo la kweli halikupatikana katika vinywa vyao; wao hawana waa.
6 Nami nikaona malaika mwingine akiruka katika mbingu ya kati, naye alikuwa na habari njema idumuyo milele ili aitangaze kuwa taarifa za mteremo kwa wale wakaao juu ya dunia, na kwa kila taifa na kabila na lugha na watu, 7 akisema kwa sauti kubwa: “Hofuni Mungu na kumpa utukufu, kwa sababu saa ya hukumu yake imewasili, na kwa hiyo mwabuduni Yeye aliyezifanya mbingu na dunia na bahari na mabubujiko ya maji.”
8 Na mwingine, malaika wa pili, akafuata, akisema: “Ameanguka! Babiloni Mkubwa ameanguka, yeye aliyefanya mataifa yote yanywe kutokana na divai ya hasira ya uasherati wake!”
9 Na malaika mwingine, wa tatu, akawafuata hao, akisema kwa sauti kubwa: “Ikiwa yeyote aabudu hayawani-mwitu na sanamu yake, na apokea alama juu ya kipaji cha uso wake au juu ya mkono wake, 10 yeye atakunywa pia kutokana na divai ya hasira ya Mungu imwagwayo bila kutoholewa ndani ya kikombe cha hasira ya kisasi yake, naye hakika atateswa-teswa kwa moto na sulfa machoni pa malaika watakatifu na machoni pa Mwana-Kondoo. 11 Na moshi wa kuteswa-teswa kwao hupanda milele na milele, na mchana na usiku hawana pumziko lolote, wale ambao huabudu hayawani-mwitu na sanamu yake, na yeyote yule apokeaye alama ya jina lake. 12 Hapa ndipo humaanisha uvumilivu kwa watakatifu, wale washikao amri za Mungu na imani kwa Yesu.”
13 Nami nikasikia sauti kutoka mbinguni ikisema: “Andika: Wenye furaha ni wafu wafao katika muungano na Bwana tangu wakati huu na kuendelea. Ndiyo, yasema roho, acheni wapumzike kutokana na kazi zao za jasho, kwa maana mambo waliyotenda yaenda yakiambatana nao moja kwa moja.”
14 Nami nikaona, na, tazama! wingu jeupe, na juu ya wingu mtu fulani kama mwana wa binadamu ameketi, mwenye taji la dhahabu juu ya kichwa chake na mundu mkali katika mkono wake.
15 Na malaika mwingine akaibuka kutoka katika patakatifu pa hekalu, kwa sauti kubwa akilia kwa yeye aketiye juu ya wingu: “Tia ndani mundu wako uvune, kwa sababu saa imekuja ya kuvuna, kwa maana mavuno ya dunia yameiva kabisa.” 16 Na yeye aketiye juu ya wingu akatia ndani mundu wake juu ya dunia, na dunia ikavunwa.
17 Na bado malaika mwingine akaibuka kutoka katika patakatifu pa hekalu palipo mbinguni, yeye, pia, akiwa na mundu mkali.
18 Na bado malaika mwingine akaibuka kutoka katika madhabahu naye alikuwa na mamlaka juu ya moto. Naye akapaaza kilio kwa sauti kubwa akamwita yule aliyekuwa na mundu mkali, akisema: “Tia ndani mundu wako mkali ukusanye vichala vya mzabibu wa dunia, kwa sababu zabibu za huo zimekuwa mbivu.” 19 Naye huyo malaika akatia mundu wake katika dunia akakusanya mzabibu wa dunia, na kuuvurumisha ndani ya sindikio kubwa la divai la hasira ya Mungu. 20 Nalo sindikio la divai likakanyagwa nje ya jiji, na damu ikatoka katika hilo sindikio la divai kufika juu kwenye hatamu za farasi, kwa umbali wa stadia elfu moja mia sita.