Ufunuo
19 Baada ya mambo haya nikasikia kilichokuwa kama sauti kubwa ya umati mkubwa mbinguni. Walisema: “Sifuni Yah, nyinyi watu! Wokovu na utukufu na nguvu ni za Mungu wetu, 2 kwa sababu hukumu zake ni za kweli na za uadilifu. Kwa maana ametekeleza hukumu juu ya kahaba mkubwa aliyeifisidi dunia kwa uasherati wake, na amelipizia kisasi damu ya watumwa wake mkononi mwake.” 3 Na saa hiyohiyo kwa mara ya pili wakasema: “Sifuni Yah, nyinyi watu! Na moshi kutoka kwake waendelea kupanda milele na milele.”
4 Na wazee ishirini na wanne na viumbe hai wanne wakaanguka chini na kuabudu Mungu aketiye juu ya kiti cha ufalme, wakasema: “Ameni! Sifuni Yah, nyinyi watu!”
5 Pia, sauti ikatoka katika kiti cha ufalme na kusema: “Mwe mkisifu Mungu wetu, nyinyi nyote watumwa wake, ambao humhofu yeye, wadogo na wakubwa.”
6 Nami nikasikia kilichokuwa kama sauti ya umati mkubwa na kama mvumo wa maji mengi na kama mvumo wa ngurumo zilizo nzito. Wakasema: “Sifuni Yah, nyinyi watu, kwa sababu Yehova Mungu wetu, Mweza-Yote, ameanza kutawala akiwa mfalme. 7 Acheni tushangilie na kuwa wenye shangwe mno, na acheni tumpe yeye utukufu, kwa sababu ndoa ya Mwana-Kondoo imewasili na mke wake amejitayarisha mwenyewe. 8 Ndiyo, amepewa ruhusa ya kupambwa kitani nyangavu, safi, bora, kwa maana hiyo kitani bora husimamia matendo ya uadilifu ya watakatifu.”
9 Naye aniambia mimi: “Andika: Wenye furaha ni wale walioalikwa kwenye mlo wa jioni wa ndoa ya Mwana-Kondoo.” Pia, aniambia mimi: “Hizo ni semi za kweli za Mungu.” 10 Ndipo nikaanguka chini mbele ya miguu yake kumwabudu yeye. Lakini yeye aniambia: “Uwe mwangalifu! Usifanye hivyo! Mimi ni mtumwa tu mwenzako na wa ndugu zako walio na kazi ya kutoa ushahidi kuhusu Yesu. Abudu Mungu; kwa maana kutoa ushahidi kuhusu Yesu ndiko hupulizia kutoa unabii.”
11 Nami nikaona mbingu imefunguliwa, na, tazama! farasi mweupe. Na yeye aketiye juu yake aitwa Mwaminifu na Wa-Kweli, naye ahukumu na kuendeleza vita katika uadilifu. 12 Macho yake ni mwali wa moto, na juu ya kichwa chake kuna vilemba vingi. Ana jina lililoandikwa ambalo hakuna yeyote alijuaye ila yeye mwenyewe, 13 naye amepambwa vazi la nje lililonyunyiziwa damu, na jina aitwalo ni Neno la Mungu. 14 Pia, majeshi yaliyokuwa mbinguni yalikuwa yakimfuata juu ya farasi weupe, nayo yalikuwa yamevikwa kitani nyeupe, safi, bora. 15 Na kutoka kinywani mwake hutokeza upanga mrefu mkali, ili apate kupiga mataifa kwa huo, naye atawachunga kwa fimbo ya chuma. Yeye akanyaga pia sindikio la divai ya hasira ya hasira-kisasi ya Mungu Mweza-Yote. 16 Na juu ya vazi lake la nje, hata juu ya paja lake, ana jina ambalo limeandikwa, Mfalme wa wafalme na Bwana wa mabwana.
17 Nikaona pia malaika amesimama katika jua, naye akapaaza kilio kwa sauti kubwa na kuwaambia ndege wote warukao katika mbingu ya kati: “Njoni hapa, mkusanyike pamoja kwenye mlo wa jioni wa Mungu ulio mkubwa, 18 ili mpate kula sehemu zenye nyama za wafalme na sehemu zenye nyama za makamanda wa kijeshi na sehemu zenye nyama za watu wenye nguvu na sehemu zenye nyama za farasi na za hao waketio juu yao, na sehemu zenye nyama za wote, za watu huru na vilevile za watumwa na za wadogo na wakubwa.”
19 Nami nikaona hayawani-mwitu na wafalme wa dunia na majeshi yao wamekusanyika pamoja kufanya vita na yeye aketiye juu ya farasi na jeshi lake. 20 Na hayawani-mwitu akashikwa, na pamoja naye nabii asiye wa kweli aliyefanya mbele yake ishara ambazo kwazo aliongoza vibaya wale waliopokea alama ya hayawani-mwitu na wale ambao hutolea sanamu yake ibada. Huku wakiwa bado hai, wote wawili wakavurumishwa ndani ya ziwa la moto liwakalo kwa sulfa. 21 Lakini wale wengine wakauawa kabisa kwa upanga mrefu wa yeye aketiye juu ya farasi, upanga uliotoka kinywani mwake. Na ndege wote wakashiba sehemu zao zenye nyama.