Ufunuo
18 Baada ya mambo haya nikaona malaika mwingine akishuka kutoka mbinguni, mwenye mamlaka kubwa; na dunia ilinurishwa kutokana na utukufu wake. 2 Naye akapaaza kilio kwa sauti yenye nguvu, akisema: “Ameanguka! Babiloni Mkubwa ameanguka, na amekuwa mahali pa kukaa pa roho waovu na mahali pa kuotea pa kila mpumuo usio safi na mahali pa kuotea pa kila ndege asiye safi na mwenye kuchukiwa! 3 Kwa sababu ya divai ya hasira ya uasherati wake mataifa yote yameanguka yakiwa majeruhi, na wafalme wa dunia walifanya uasherati naye, na wafanya-biashara wanaosafiri wa dunia wakawa matajiri kwa sababu ya nguvu ya anasa yake isiyo na aibu.”
4 Nami nikasikia sauti nyingine kutoka mbinguni ikisema: “Tokeni kwake, watu wangu, ikiwa hamtaki kushiriki pamoja naye dhambi zake, na ikiwa hamtaki kupokea sehemu ya tauni zake. 5 Kwa maana dhambi zake zimetungamana pamoja hadi mbinguni, na Mungu amekumbuka matendo yake yasiyo ya haki. 6 Mlipeni sawa na vile yeye mwenyewe alivyolipa, na mfanyeni mara mbili ya kadiri ya hivyo, ndiyo, mara mbili ya hesabu ya mambo aliyoyatenda; katika kikombe ambacho yeye alitia mchanganyiko ndani yacho mtilieni mchanganyiko mara mbili ya kadiri hiyo. 7 Kwa kadiri ambayo alijitukuza mwenyewe na kuishi katika anasa isiyo na aibu, kwa kadiri hiyo mteseni-teseni na kumpa ombolezo. Kwa maana moyoni mwake afuliza kusema, ‘Naketi nikiwa malkia, nami si mjane, nami sitaona maombolezo kamwe.’ 8 Hiyo ndiyo sababu katika siku moja tauni zake zitakuja, kifo na kuomboleza na njaa kali, naye atachomwa kabisa kwa moto, kwa sababu Yehova Mungu, aliyemhukumu, ni mwenye nguvu.
9 “Na wafalme wa dunia waliofanya uasherati naye na kuishi katika anasa isiyo na aibu watatoa machozi na kujipiga wenyewe kwa kihoro juu yake, watazamapo moshi uliotokana na kuungua kwake, 10 wakiwa wamesimama umbali fulani kwa sababu ya hofu yao ya kuteswa-teswa kwake na kusema, ‘Ole, ole, wewe jiji kubwa, Babiloni wewe jiji lenye nguvu, kwa sababu katika saa moja hukumu yako imewasili!’
11 “Pia, wafanya-biashara wa dunia wanaosafiri wanatoa machozi na kuomboleza juu yake, kwa sababu hakuna yeyote wa kununua tena kamwe bidhaa zao zilizojaa, 12 bidhaa zilizojaa za dhahabu na fedha na jiwe lenye bei na lulu na kitani bora na zambarau na hariri na nyekundu-nyangavu; na kila kitu cha miti iliyotiwa mnukio na kila namna ya kitu cha pembe ya tembo na kila namna ya kitu kitokanacho na miti yenye bei zaidi sana na cha shaba na cha chuma na cha marumaru; 13 pia dalasini na kiungo cha Kihindi na uvumba na mafuta yenye marashi na ubani na divai na mafuta ya zeituni na unga bora na ngano na ng’ombe na kondoo, na farasi na magari na watumwa na nafsi za kibinadamu. 14 Ndiyo, tunda bora ambalo nafsi yako ilitamani limeondoka kwako, na vitu vyote vitamu na vitu vyenye kung’ara vimeangamia kutoka kwako, na watu hawatavipata tena kamwe.
15 “Wafanya-biashara wanaosafiri wa vitu hivyo, waliopata kuwa matajiri kutokana naye, watasimama umbali fulani kwa sababu ya hofu yao juu ya kuteswa-teswa kwake na watatoa machozi na kuomboleza, 16 wakisema, ‘Ole, ole —jiji kubwa, lililovishwa kitani bora na zambarau na nyekundu-nyangavu, na kurembwa kitajiri kwa madoido ya dhahabu na mawe yenye bei na lulu, 17 kwa sababu katika saa moja mali nyingi hivyo zimefanywa ukiwa!’
“Na kila kapteni wa meli na kila mtu ambaye husafiri baharini popote, na mabaharia na wale wote ambao hupata riziki kwa bahari, walisimama umbali fulani 18 na kupaaza kilio walipokuwa wakiutazama moshi uliotokana na kuchomwa moto kwake na kusema, ‘Ni jiji gani lililo kama jiji kubwa hili?’ 19 Nao wakatupa mavumbi juu ya vichwa vyao na kupaaza kilio, wakitoa machozi na kuomboleza, na kusema, ‘Ole, ole, —jiji kubwa, ambalo katika hilo wote walio na mashua baharini walipata kuwa matajiri kwa sababu yalo kuwa ni la gharama kubwa, kwa sababu katika saa moja amefanywa ukiwa!’
20 “Terema juu yake, Ewe mbingu, pia nyinyi watakatifu na nyinyi mitume na nyinyi manabii, kwa sababu kwa hukumu Mungu amemtoza adhabu kwa ajili yenu!”
21 Na malaika mwenye nguvu akainua jiwe kama jiwe kubwa la kusagia na kulivurumisha ndani ya bahari, akisema: “Hivyo kwa mtupo wa kasi sana atavurumishwa chini Babiloni lile jiji kubwa, na hatapatikana tena kamwe. 22 Na mvumo wa waimbaji ambao hufuatanisha sauti zao wenyewe kwa kinubi na wa wanamuziki na wa wapiga-filimbi na wa wapiga-tarumbeta hautasikiwa tena kamwe katika wewe, na hakuna msanii wa kazi yoyote atakayepatikana wakati wowote tena katika wewe, na hakuna mvumo wa jiwe la kusagia utakaosikiwa tena kamwe katika wewe, 23 na hakuna nuru ya taa itakayong’aa tena kamwe katika wewe, na hakuna sauti yoyote ya bwana-arusi na bibi-arusi itakayosikiwa tena kamwe katika wewe; kwa sababu wafanya-biashara wako wanaosafiri walikuwa watu wenye daraja la juu wa dunia, kwa maana kwa zoea lako la kuwasiliana na roho mataifa yote yaliongozwa vibaya. 24 Ndiyo, katika yeye ilipatikana damu ya manabii na ya watakatifu na ya wote wale ambao wamechinjwa juu ya dunia.”