Ufunuo
20 Nami nikaona malaika akiteremka kutoka mbinguni mwenye ufunguo wa abiso na mnyororo mkubwa mkononi mwake. 2 Naye akalikamata joka kubwa, nyoka wa awali, aliye Ibilisi na Shetani, na kumfunga kwa miaka elfu. 3 Naye akamvurumisha ndani ya abiso na kuifunga na kuitia muhuri juu yake, ili asipate kuongoza mataifa vibaya tena kamwe mpaka miaka elfu ilipokuwa imekwisha. Baada ya mambo haya lazima yeye afunguliwe kwa muda kidogo.
4 Nami nikaona viti vya ufalme, na kulikuwa na wale walioketi juu yavyo, nao wakapewa mamlaka ya kuhukumu. Ndiyo, mimi nikaona nafsi za wale waliouawa kwa shoka kwa ajili ya ushahidi waliotoa kuhusu Yesu na kwa ajili ya kusema juu ya Mungu, na wale ambao hawakuwa wameabudu wala hayawani-mwitu wala sanamu yake na ambao hawakuwa wamepokea alama juu ya kipaji cha uso wao na juu ya mkono wao. Nao wakaja kwenye uhai wakatawala wakiwa wafalme pamoja na Kristo kwa miaka elfu. 5 (Wale wafu waliosalia hawakuja kwenye uhai mpaka miaka elfu ilipokuwa imekwisha.) Huu ndio ufufuo wa kwanza. 6 Mwenye furaha na mtakatifu ni yeyote aliye na sehemu katika ufufuo wa kwanza; juu ya hao kifo cha pili hakina mamlaka yoyote, bali watakuwa makuhani wa Mungu na wa Kristo, na watatawala wakiwa wafalme pamoja naye kwa miaka elfu.
7 Sasa mara tu miaka elfu iishapo, Shetani atafunguliwa kutoka katika gereza lake, 8 naye atatoka kwenda kuyaongoza vibaya yale mataifa katika pembe nne za dunia, Gogu na Magogu, kuyakusanya pamoja kwa ajili ya vita. Hesabu yayo ni kama mchanga wa bahari. 9 Nayo yakasonga juu ya upana wa dunia na kuizunguka kambi ya watakatifu na jiji lenye kupendwa. Lakini moto ukateremka kutoka mbinguni ukayameza. 10 Naye Ibilisi aliyekuwa akiyaongoza vibaya alivurumishwa ndani ya ziwa la moto na sulfa, ambamo wote wawili hayawani-mwitu na nabii asiye wa kweli tayari walikuwamo; nao watateswa-teswa mchana na usiku milele na milele.
11 Nami nikaona kiti cha ufalme kikubwa cheupe na yeye aketiye juu yacho. Kutoka mbele yake dunia na mbingu zikakimbilia mbali, na hakuna mahali palipopatikana kwa ajili yazo. 12 Nami nikaona wafu, wakubwa na wadogo, wamesimama mbele ya hicho kiti cha ufalme, na hati-kunjo zikafunguliwa. Lakini hati-kunjo nyingine ikafunguliwa; hiyo ndiyo hati-kunjo ya uhai. Na hao wafu wakahukumiwa kutokana na mambo yale yaliyoandikwa katika hizo hati-kunjo kulingana na vitendo vyao. 13 Nayo bahari ikawatoa hao wafu waliokuwa ndani yayo, na kifo na Hadesi vikawatoa wafu ndani yavyo, nao walihukumiwa mmoja-mmoja kulingana na vitendo vyao. 14 Na kifo na Hadesi vikavurumishwa ndani ya ziwa la moto. Hili humaanisha kifo cha pili, ziwa la moto. 15 Zaidi ya hilo, yeyote yule ambaye hakupatikana ameandikwa katika kitabu cha uhai alivurumishwa ndani ya ziwa la moto.