Mathayo
19 Basi Yesu alipokuwa amemaliza maneno hayo, aliondoka Galilaya na kuja kwenye mipaka ya Yudea ng’ambo ya Yordani. 2 Pia, umati mkubwa ulimfuata, naye akauponya huko.
3 Na Mafarisayo wakamjia, wakikusudia kumshawishi na kusema: “Je, yaruhusika kisheria mtu kutaliki mke wake kwa kila namna ya sababu?” 4 Kwa kujibu akasema: “Je, hamkusoma kwamba yeye aliyewaumba wao kutoka mwanzo aliwafanya wa kiume na wa kike 5 na kusema, ‘Kwa sababu hiyo mtu ataacha baba yake na mama yake naye atashikamana na mke wake, na hao wawili watakuwa mwili mmoja’? 6 Hivi kwamba wao si wawili tena, bali mwili mmoja. Kwa hiyo, kile ambacho Mungu amefunga nira pamoja msiache mtu yeyote akitenganishe.” 7 Wakamwambia: “Basi, kwa nini, Musa aliagiza kutoa cheti cha kufukuza na kutaliki mke?” 8 Akawaambia: “Musa, kwa kufikiria ugumu wenu wa moyo, aliwatolea idhini ya kuwataliki wake zenu, lakini haijawa hivyo kutoka mwanzo. 9 Nawaambia kwamba yeyote yule atalikiye mke wake, ila kwa sababu ya uasherati, na kuoa mwingine afanya uzinzi.”
10 Wanafunzi wakamwambia: “Ikiwa hali iko namna hiyo ya mwanamume pamoja na mke wake, haifai kuoa.” 11 Yeye akawaambia: “Si watu wote wafanyao nafasi kwa huo usemi, ila tu wale walio na hiyo zawadi. 12 Kwa maana kuna matowashi waliozaliwa namna hiyo kutoka katika tumbo la uzazi la mama yao, na kuna matowashi waliofanywa matowashi na watu, na kuna matowashi ambao wamejifanya wenyewe matowashi kwa sababu ya ufalme wa mbingu. Acheni yeye awezaye kufanyia hilo nafasi alifanyie hilo nafasi.”
13 Ndipo watoto wachanga wakaletwa kwake, ili aweke mikono yake juu yao na kutoa sala; lakini wanafunzi wakawakemea. 14 Hata hivyo, Yesu akasema: “Waacheni watoto wachanga, na komeni kuwazuia kunijia, kwa maana ufalme wa mbingu ni wa walio kama hao.” 15 Naye akaweka mikono yake juu yao na kwenda kutoka hapo.
16 Sasa, tazama! mtu fulani alimjia na kusema: “Mwalimu, ni lazima nifanye wema gani kusudi nipate uhai udumuo milele?” 17 Yeye akamwambia: “Kwa nini waniuliza juu ya lililo jema? Mmoja yuko aliye mwema. Ingawa hivyo, ikiwa wataka kuingia katika uhai, zishike amri kwa kuendelea.” 18 Akamwambia: “Zipi?” Yesu akasema: “Naam, Lazima usiue kimakusudi, Lazima usifanye uzinzi, Lazima usiibe, Lazima usitoe ushahidi usio wa kweli, 19 Heshimu baba yako na mama yako, na, Lazima upende jirani yako kama wewe mwenyewe.” 20 Huyo mwanamume kijana akamwambia: “Nimeyashika yote hayo; ni nini bado ninachokosa?” 21 Yesu akamwambia: “Ikiwa wataka kuwa mkamilifu, nenda ukauze mali zako na uwape maskini nawe utakuwa na hazina mbinguni, na uje uwe mfuasi wangu.” 22 Huyo mwanamume kijana aliposikia usemi huo, akaenda zake akiwa ametiwa kihoro, kwa maana alikuwa na miliki nyingi. 23 Lakini Yesu akawaambia wanafunzi wake: “Kwa kweli nawaambia nyinyi kwamba litakuwa jambo gumu kwa mtu tajiri kuingia katika ufalme wa mbingu. 24 Tena nawaambia nyinyi, Ni rahisi zaidi ngamia kupita katika tundu la sindano kuliko kwa mtu tajiri kupata kuingia katika ufalme wa Mungu.”
25 Wanafunzi waliposikia hilo, walionyesha mshangao mkubwa, wakisema: “Ni nani kwa kweli awezaye kuokolewa?” 26 Akiwatazama usoni, Yesu akawaambia: “Kwa wanadamu hilo haliwezekani, bali kwa Mungu mambo yote yawezekana.”
27 Ndipo Petro akamwambia kwa kujibu: “Tazama! Sisi tumeacha vitu vyote na kukufuata wewe; kwa kweli kutakuwa nini kwa ajili yetu?” 28 Yesu akawaambia: “Kwa kweli nawaambia nyinyi, Katika uumbaji-upya wakati Mwana wa binadamu aketipo juu ya kiti chake cha ufalme chenye utukufu, nyinyi ambao mmenifuata mtaketi nyinyi wenyewe pia juu ya viti vya ufalme kumi na viwili, mkihukumu yale makabila kumi na mawili ya Israeli. 29 Na kila mtu ambaye ameziacha nyumba au kuacha akina ndugu au akina dada au baba au mama au watoto au mashamba kwa ajili ya jina langu atapokea mara nyingi zaidi naye atarithi uhai udumuo milele.
30 “Lakini wengi walio wa kwanza watakuwa wa mwisho na wa mwisho wawe wa kwanza.