Mathayo
16 Hapa Mafarisayo na Masadukayo wakamkaribia na, ili kumshawishi, wakamuuliza awaonyeshe ishara kutoka mbinguni. 2 Kwa kujibu akawaambia: “[[Iwapo jioni nyinyi huwa na desturi ya kusema, ‘Itakuwa hali-hewa nzuri, kwa maana anga ni nyekundu-moto’; 3 na kwenye asubuhi, ‘Itakuwa hali-hewa ya baridi-baridi, yenye mvua-mvua leo, kwa maana anga ni nyekundu-moto, lakini yenye sura nzito-nzito.’ Mwajua jinsi ya kufasiri kuonekana kwa anga, lakini ishara za nyakati hamwezi kuzifasiri.]] 4 Kizazi kiovu na chenye uzinzi hufuliza kutafuta ishara, lakini hakuna ishara kitakayopewa ila ile ishara ya Yona.” Ndipo akaenda zake, akiwaacha nyuma.
5 Sasa wanafunzi wakavuka mpaka ule upande mwingine na kusahau kuichukua mikate. 6 Yesu akawaambia: “Fulizeni kufungua macho yenu na jiangalieni na chachu ya Mafarisayo na Masadukayo.” 7 Kwa hiyo wakaanza kuwazawaza miongoni mwao wenyewe, wakisema: “Hatukuchukua mikate yoyote pamoja nasi.” 8 Akijua hilo, Yesu akasema: “Kwa nini mnafanya kuwazawaza huku miongoni mwenu wenyewe, kwa sababu hamna mikate, nyinyi wenye imani kidogo? 9 Je, bado hamwioni maana, au je, hamkumbuki ile mikate mitano katika kisa cha wale elfu tano na ni vikapu vingapi mlivyookota? 10 Au ile mikate saba katika kisa cha wale elfu nne na ni makapu mangapi ya chakula mliyookota? 11 Ni jinsi gani hamfahamu kwamba sikuongea nanyi juu ya mikate? Bali jihadharini na chachu ya Mafarisayo na Masadukayo.” 12 Ndipo wakafahamu kwamba alisema juu ya kujiangalia, si na chachu ya ile mikate, bali na fundisho la Mafarisayo na Masadukayo.
13 Sasa alipokuwa amekuja kuingia katika sehemu za Kaisaria Filipi, Yesu alianza kuuliza wanafunzi wake: “Watu wanasema Mwana wa binadamu ni nani?” 14 Wao wakasema: “Baadhi yao husema Yohana Mbatizaji, wengine Eliya, bado wengine Yeremia au mmoja wa manabii.” 15 Akawaambia: “Ingawa hivyo, nyinyi mwasema mimi ni nani?” 16 Kwa kujibu Simoni Petro akasema: “Wewe ndiwe Kristo, Mwana wa Mungu aliye hai.” 17 Kwa kujibu Yesu akamwambia: “Mwenye furaha ni wewe, Simoni mwana wa Yona, kwa sababu nyama na damu havikukufunulia hilo, bali Baba yangu aliye katika mbingu ndiye aliyekufunulia. 18 Pia, nakuambia, Wewe ni Petro, na juu ya tungamo-mwamba hili hakika nitajenga kutaniko langu, na malango ya Hadesi hayatalizidi nguvu. 19 Hakika nitakupa wewe funguo za ufalme wa mbingu, na lolote lile ambalo huenda ukafunga juu ya dunia litakuwa ndilo jambo lililofungwa katika mbingu, na lolote lile ambalo huenda wewe ukafungua juu ya dunia litakuwa ndilo jambo lililofunguliwa katika mbingu.” 20 Ndipo akawaagiza wanafunzi kwa kusisitiza wasiambie yeyote kwamba yeye ni Kristo.
21 Tangu wakati huo na kuendelea Yesu Kristo akaanza kuwaonyesha wanafunzi wake kwamba ni lazima yeye aende Yerusalemu na kupatwa na mambo mengi kutoka kwa wanaume wazee na makuhani wakuu na waandishi, na kuuawa, na siku ya tatu afufuliwe. 22 Ndipo Petro akamchukua kando na kuanza kumkemea, akisema: “Uwe mwenye fadhili kwako mwenyewe, Bwana; wewe hutapatwa hata kidogo na jambo hili.” 23 Lakini, akigeuza mgongo wake, yeye akamwambia Petro: “Nenda nyuma yangu, Shetani! Wewe ni kipingamizi chenye kukwaza kwangu, kwa sababu wewe wafikiri, si fikira za Mungu, bali zile za wanadamu.”
24 Ndipo Yesu akawaambia wanafunzi wake: “Ikiwa yeyote ataka kunifuata, na ajikane mwenyewe na kuchukua mti wake wa mateso na kunifuata kwa kuendelea. 25 Kwa maana yeyote yule atakaye kuokoa nafsi yake ataipoteza; lakini yeyote yule aipotezaye nafsi yake kwa ajili yangu ataipata. 26 Kwa maana itakuwa manufaa gani kwa mtu ikiwa atapata faida ya kuwa na ulimwengu wote lakini aipoteze nafsi yake? au ni nini mtu atatoa katika kubadilishana kwa ajili ya nafsi yake? 27 Kwa maana Mwana wa binadamu akusudiwa kuja katika utukufu wa Baba yake pamoja na malaika zake, na ndipo atakapomlipa kila mmoja kulingana na mwenendo wake. 28 Kwa kweli nawaambia nyinyi kwamba kuna baadhi ya wale ambao wamesimama hapa ambao hawataonja kifo hata kidogo mpaka kwanza wamwone Mwana wa binadamu akija katika ufalme wake.”