Mathayo
5 Alipouona umati alipanda kwenda katika mlima; na baada ya yeye kuketi wanafunzi wake wakamjia; 2 naye akafungua kinywa chake na kuanza kuwafundisha, akisema:
3 “Wenye furaha ni wale wenye kuona uhitaji wao wa kiroho, kwa kuwa ufalme wa mbingu ni wao.
4 “Wenye furaha ni wale ambao huomboleza, kwa kuwa wao watafarijiwa.
5 “Wenye furaha ni wenye tabia-pole, kwa kuwa wao watairithi dunia.
6 “Wenye furaha ni wale walio na njaa na walio na kiu kwa ajili ya uadilifu, kwa kuwa wao watashibishwa.
7 “Wenye furaha ni wenye rehema, kwa kuwa wao wataonyeshwa rehema.
8 “Wenye furaha ni wenye kutakata moyoni, kwa kuwa wao watamwona Mungu.
9 “Wenye furaha ni wenye kufanya amani, kwa kuwa wao wataitwa ‘wana wa Mungu.’
10 “Wenye furaha ni wale ambao wamenyanyaswa kwa ajili ya uadilifu, kwa kuwa ufalme wa mbingu ni wao.
11 “Wenye furaha ni nyinyi watu wawashutumupo na kuwanyanyasa nyinyi na kusema kwa uwongo kila namna ya jambo ovu dhidi yenu kwa ajili yangu. 12 Shangilieni na kuruka kwa shangwe, kwa kuwa thawabu yenu ni kubwa katika mbingu; kwa maana katika njia hiyo waliwanyanyasa manabii waliokuwa kabla yenu.
13 “Nyinyi ndio chumvi ya dunia; lakini ikiwa chumvi yapoteza nguvu yayo, uchumvi wayo utarudishwaje? Si yenye kutumika tena kwa kitu chochote bali ni ya kutupwa nje ili kukanyagwa-kanyagwa na watu.
14 “Nyinyi ndio nuru ya ulimwengu. Jiji haliwezi kufichwa liwapo limesimama juu ya mlima. 15 Watu huwasha taa na kuiweka, si chini ya kikapu cha kupimia, bali juu ya kinara cha taa, nayo hung’aa juu ya wote walio katika nyumba. 16 Hivyohivyo acheni nuru yenu ing’ae mbele ya watu, ili wapate kuona kazi zenu bora na kumpa utukufu Baba yenu aliye katika mbingu.
17 “Msifikiri nilikuja kuharibu Sheria au Manabii. Nilikuja, si kuharibu, bali kutimiza; 18 kwa maana kwa kweli nawaambia nyinyi kwamba mbingu na dunia zingepitilia mbali upesi zaidi kuliko kwa herufi moja ndogo zaidi sana au nukta moja ya herufi kupitilia mbali kutoka katika Sheria kwa vyovyote na mambo yote yasitukie. 19 Kwa hiyo, yeyote yule avunjaye moja ya amri hizi ndogo zaidi sana na kufundisha wanadamu hivyo, yeye ataitwa ‘mdogo zaidi sana’ kuhusiana na ufalme wa mbingu. Kwa habari ya yeyote azifanyaye na kuzifundisha, huyo ataitwa ‘mkubwa’ kuhusiana na ufalme wa mbingu. 20 Kwa maana nawaambia nyinyi kwamba ikiwa uadilifu wenu hauzidi ule wa waandishi na Mafarisayo, hamtaingia kwa vyovyote katika ufalme wa mbingu.
21 “Nyinyi mlisikia kwamba ilisemwa kwa wale wa nyakati za kale, ‘Lazima usiue kimakusudi; lakini yeyote yule afanyaye uuaji-kimakusudi atapaswa kutoa hesabu kwa mahakama ya kuamulia haki.’ 22 Hata hivyo, mimi nawaambia nyinyi kwamba kila mtu aendeleaye kuwa na hasira ya kisasi na ndugu yake atapaswa kutoa hesabu kwa mahakama ya kuamulia haki; lakini yeyote yule amwambiaye ndugu yake neno la dharau lisilosemeka atapaswa kutoa hesabu kwa Mahakama Kuu Zaidi; hali yeyote yule asemaye, ‘Wewe baradhuli!’ atakuwa mwenye kustahili Gehena ya moto.
23 “Basi, ikiwa wewe unaleta zawadi yako kwenye madhabahu na huko wakumbuka kwamba ndugu yako ana jambo fulani dhidi yako, 24 acha zawadi yako hapo mbele ya madhabahu, na uende zako; kwanza fanya amani yako na ndugu yako, na ndipo, ukiisha kurudi, toa zawadi yako.
25 “Uwe na nia ya kusuluhisha mambo upesi pamoja na mlalamishi wako anayekushtaki mahakamani, wakati wewe uwapo pamoja naye njiani kwenda huko, ili kwa njia fulani mlalamikaji asipate kukukabidhi kwa hakimu, naye hakimu kwa hadimu wa mahakama, nawe utupwe ndani ya gereza. 26 Nakuambia kwa kweli, Hakika wewe hutatoka humo mpaka uwe umemaliza kulipa sarafu ya mwisho ya thamani ndogo sana.
27 “Nyinyi mlisikia kwamba ilisemwa, ‘Lazima usifanye uzinzi.’ 28 Lakini mimi nawaambia nyinyi kwamba kila mtu ambaye hufuliza kumtazama mwanamke ili kuwa na harara kwa ajili yake tayari amefanya uzinzi pamoja naye moyoni mwake. 29 Ikiwa, sasa, jicho lako hilo la kuume linakufanya ukwazike, ling’oe kabisa na ulitupilie mbali nawe. Kwa maana ni manufaa zaidi kwako kimoja cha viungo vyako kipotee kwako kuliko mwili wako wote kutupwa katika Gehena. 30 Pia, ikiwa mkono wako wa kuume unakufanya ukwazike, ukatilie mbali na kuutupilia mbali nawe. Kwa maana ni manufaa zaidi kwako kimoja cha viungo vyako kipotee kuliko mwili wako wote kuanguka katika Gehena.
31 “Zaidi ya hayo ilisemwa, ‘Yeyote yule atalikiye mke wake, acheni ampe cheti cha talaka.’ 32 Hata hivyo, mimi nawaambia nyinyi kwamba kila mtu anayetaliki mke wake, ila kwa sababu ya uasherati, amfanya aelekee kufanya uzinzi, na yeyote yule aoaye mwanamke aliyetalikiwa afanya uzinzi.
33 “Tena mlisikia kwamba ilisemwa kwa wale wa nyakati za kale, ‘Lazima usiape bila kutimiza, bali lazima ulipe nadhiri zako kwa Yehova.’ 34 Hata hivyo, mimi nawaambia nyinyi: Msiape hata kidogo, wala kwa mbingu, kwa sababu ni kiti cha ufalme cha Mungu; 35 wala kwa dunia, kwa sababu ndicho kibago cha miguu yake; wala kwa Yerusalemu, kwa sababu ndilo jiji la yule Mfalme mkubwa. 36 Wala kwa kichwa chako lazima usiape, kwa sababu huwezi kugeuza unywele mmoja kuwa mweupe au mweusi. 37 Acheni tu neno lenu Ndiyo limaanishe Ndiyo, La yenu, La; kwa maana lizidilo hayo ni kutoka kwa yule mwovu.
38 “Nyinyi mlisikia kwamba ilisemwa, ‘Jicho kwa jicho na jino kwa jino.’ 39 Hata hivyo, mimi nawaambia nyinyi: Msimkinze yeye aliye mwovu; bali yeyote akupigaye kofi kwenye shavu lako la kuume, mgeuzie lile jingine pia. 40 Na ikiwa mtu ataka kwenda mahakamani pamoja nawe na kupata umiliki wa vazi lako la ndani, acha vazi lako la nje pia limwendee; 41 na ikiwa mtu fulani aliye chini ya mamlaka akushurutisha ufanye utumishi kwa kilometa moja, nenda pamoja naye kilometa mbili. 42 Mpe yeye anayekuomba, na usigeuke kutoka kwake atakaye kuazima kutoka kwako pasipo faida.
43 “Nyinyi mlisikia kwamba ilisemwa, ‘Lazima umpende jirani yako na kuchukia adui yako.’ 44 Hata hivyo, mimi nawaambia nyinyi: Endeleeni kupenda maadui wenu na kusali kwa ajili ya wale wanaowanyanyasa nyinyi; 45 ili mpate kujithibitisha wenyewe kuwa wana wa Baba yenu aliye katika mbingu, kwa kuwa yeye hufanya jua lake lichomoze juu ya watu waovu na wema na kufanya mvua inyeshe juu ya watu waadilifu na wasio waadilifu. 46 Kwa maana mkipenda wale wanaowapenda nyinyi, mna thawabu gani? Je, wakusanya-kodi pia hawafanyi jambo hilohilo? 47 Na mkisalimu ndugu zenu tu, ni jambo gani lizidilo la kawaida mnalofanya? Je, watu wa mataifa pia hawafanyi jambo hilohilo? 48 Lazima nyinyi basi mwe wakamilifu, kama Baba yenu wa kimbingu alivyo mkamilifu.