Mathayo
24 Akiondoka sasa, Yesu akawa ameshika njia yake kutoka hekaluni, lakini wanafunzi wake wakamkaribia kumwonyesha majengo ya hekalu. 2 Kwa kujibu akawaambia: “Je, hamvioni vitu vyote hivi? Kwa kweli nawaambia nyinyi, Kwa vyovyote halitaachwa jiwe juu ya jiwe hapa na lisiangushwe chini.”
3 Alipokuwa ameketi juu ya Mlima wa Mizeituni, wanafunzi walimkaribia kwa faragha, wakisema: “Tuambie, Ni wakati gani mambo haya yatakuwa, nayo itakuwa ni nini ishara ya kuwapo kwako na ya umalizio wa mfumo wa mambo?”
4 Na kwa kujibu Yesu akawaambia: “Jihadharini kwamba mtu yeyote asiwaongoze nyinyi vibaya; 5 kwa maana wengi watakuja juu ya msingi wa jina langu, wakisema, ‘Mimi ndiye Kristo,’ nao wataongoza wengi vibaya. 6 Mtasikia juu ya vita na ripoti za vita; angalieni kwamba hamwogofishwi. Kwa maana mambo haya lazima yatukie, lakini mwisho bado.
7 “Kwa maana taifa litainuka dhidi ya taifa na ufalme dhidi ya ufalme, na kutakuwa na upungufu wa chakula na matetemeko ya dunia mahali pamoja baada ya pengine. 8 Mambo yote hayo ni mwanzo wa maumivu makali ya ghafula ya taabu.
9 “Ndipo watu watakapowakabidhi nyinyi kwenye dhiki na watawaua nyinyi, nanyi mtakuwa vitu vya kuchukiwa na mataifa yote kwa sababu ya jina langu. 10 Ndipo, pia, wengi watakapokwazika na watasalitiana na watachukiana. 11 Na manabii wengi wasio wa kweli watainuka na kuongoza wengi vibaya; 12 na kwa sababu ya kuongezeka kwa uasi-sheria upendo wa idadi iliyo kubwa zaidi utapoa. 13 Lakini yeye ambaye amevumilia hadi mwisho ndiye atakayeokolewa. 14 Na habari njema hii ya ufalme itahubiriwa katika dunia yote inayokaliwa kwa ajili ya kuwa ushahidi kwa mataifa yote; na ndipo mwisho utakapokuja.
15 “Kwa hiyo, mwonapo mara hiyo kitu chenye kuchukiza sana ambacho husababisha ukiwa, kama kilivyosemwa kupitia Danieli nabii, kikiwa kimesimama katika mahali patakatifu, (mwacheni msomaji atumie ufahamu,) 16 ndipo waacheni wale walio katika Yudea waanze kukimbilia milimani. 17 Mwacheni mtu aliye juu ya paa ya nyumba asiteremke kuzichukua mali kutoka katika nyumba yake; 18 na mwacheni mtu aliye katika shamba asirudi kwenye nyumba kuchukua vazi lake la nje. 19 Ole wao wanawake wenye mimba na wale wanaonyonyesha mtoto mchanga sana katika siku hizo! 20 Fulizeni kusali kwamba kimbio lenu lisipate kutukia wakati wa majira ya baridi kali, wala siku ya sabato; 21 kwa maana ndipo kutakuwa na dhiki kubwa ya namna ambayo haijapata kutukia tangu mwanzo wa ulimwengu hadi sasa, la, wala haitatukia tena. 22 Kwa kweli, kama siku hizo hazingekatwa ziwe fupi, hakuna mwili ambao ungeokolewa; lakini kwa sababu ya wale wachaguliwa siku hizo zitakatwa ziwe fupi.
23 “Ndipo yeyote akiwaambia nyinyi, ‘Tazameni! Kristo ni huyu hapa,’ au, ‘Pale!’ msiamini hilo. 24 Kwa maana Makristo wasio wa kweli na manabii wasio wa kweli watainuka na kutoa ishara zilizo kubwa na maajabu ili kuongoza vibaya, ikiwezekana, hata wale wachaguliwa. 25 Tazameni! Nimewaonya nyinyi kimbele. 26 Kwa hiyo, watu wakiwaambia nyinyi, ‘Tazameni! Yeye yuko nyikani,’ msitoke kwenda; ‘Tazameni! Yeye yumo katika vyumba vya ndani,’ msiamini hilo. 27 Kwa maana kama vile umeme hutokea sehemu za mashariki na kung’aa hadi sehemu za magharibi, ndivyo kuwapo kwa Mwana wa binadamu kutakavyokuwa. 28 Kokote mzoga uliko, huko ndiko tai watakusanywa pamoja.
29 “Mara baada ya ile dhiki ya siku hizo jua litatiwa giza, nao mwezi hautatoa nuru yao, nazo nyota zitaanguka kutoka mbinguni, nazo nguvu za mbingu zitatikiswa. 30 Na ndipo ishara ya Mwana wa binadamu itakapoonekana mbinguni, na ndipo makabila yote ya dunia yatakapojipiga yenyewe kwa maombolezo, nayo yatamwona Mwana wa binadamu akija juu ya mawingu ya mbinguni na nguvu na utukufu mkubwa. 31 Naye atatuma malaika zake pamoja na mvumo mkubwa wa tarumbeta, nao watawakusanya wachaguliwa wake pamoja kutoka kwenye zile pepo nne, kutoka ncha moja ya mbingu hadi ncha yazo nyingine.
32 “Basi jifunzeni jambo hili kutokana na mtini kama kielezi: Mara tu tawi lao changa likuapo kuwa jororo na kutoa majani, mwajua kwamba kiangazi kiko karibu. 33 Hivyohivyo nyinyi pia, mwonapo mambo yote hayo, jueni kwamba yuko karibu milangoni. 34 Kweli nawaambia nyinyi kwamba kizazi hiki hakitapitilia mbali kwa vyovyote mpaka mambo yote haya yatukie. 35 Mbingu na dunia zitapitilia mbali, lakini maneno yangu hayatapitilia mbali kwa vyovyote.
36 “Kuhusu siku hiyo na saa hiyo hakuna mtu ajuaye, wala hao malaika wa mbingu wala Mwana, ila Baba tu. 37 Kwa maana kama vile siku za Noa zilivyokuwa, ndivyo kuwapo kwa Mwana wa binadamu kutakavyokuwa. 38 Kwa maana kama walivyokuwa katika siku hizo kabla ya furiko, wakila na kunywa, wanaume wakioa na wanawake wakiozwa, hadi siku ambayo Noa aliingia ndani ya safina; 39 nao hawakujali mpaka furiko likaja na kuwafagilia mbali wote, ndivyo kuwapo kwa Mwana wa binadamu kutakavyokuwa. 40 Wakati huo watu wawili watakuwa katika shamba: mmoja atachukuliwa na mwingine aachwe; 41 wanawake wawili watakuwa wakisaga kwenye kinu cha mkono: mmoja atachukuliwa na mwingine aachwe. 42 Kwa hiyo, fulizeni kulinda kwa sababu hamjui ni siku gani Bwana yenu anakuja.
43 “Lakini jueni jambo moja, kwamba ikiwa mwenye nyumba angalijua ni katika lindo gani mwizi anakuja, angalifuliza kuwa macho na hangaliruhusu nyumba yake ivunjwe na kuingiwa. 44 Kwa sababu hiyo nyinyi pia jithibitisheni wenyewe kuwa tayari, kwa sababu kwenye saa msiyoifikiri kuwa hiyo, Mwana wa binadamu anakuja.
45 “Ni nani kwa kweli aliye mtumwa mwaminifu na mwenye busara ambaye bwana-mkubwa wake alimweka rasmi juu ya watumishi wake wa nyumbani, kuwapa chakula chao kwa wakati ufaao? 46 Mwenye furaha ni mtumwa huyo ikiwa bwana-mkubwa wake anapowasili amkuta akifanya hivyo! 47 Kwa kweli nawaambia nyinyi, Atamweka yeye rasmi juu ya mali zake zote.
48 “Lakini ikitukia wakati wowote mtumwa mwovu huyo aseme moyoni mwake, ‘Bwana-mkubwa wangu anakawia,’ 49 na kuanza kupiga watumwa wenzake na kula na kunywa pamoja na walevi wa kupindukia, 50 bwana-mkubwa wa mtumwa huyo atakuja katika siku ambayo hatarajii na katika saa ambayo hajui, 51 naye atamwadhibu kwa ukali mkubwa zaidi na atamgawia sehemu yake pamoja na wanafiki. Huko ndiko kutoa machozi kwake na kusaga meno kwake kutakakokuwa.